1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Waasi wa M23 wazidi kukita mizizi huku diplomasia ikikwama

7 Oktoba 2025

Kundi la M23 linajikusanya na kuimarisha nguvu zake za kisiasa na kiuchumi huko mashariki mwa Kongo huku diplomasia ikishindwa. Taarifa zinasema sasa linaunda mifumo inayofanana na ya serikali ya Kinshasa.

https://p.dw.com/p/51aa7
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Rumangabo 2023 | Waasi wa M23 wajiondoa katika kambi ya kijeshi
Waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23) wakiondoka kwenye kambi ya kijeshi ya Rumangabo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 6, 2023.Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Kundi la M23 linaripotiwa kusajili wanajeshi, kuwatoza wakaazi kodi na kuwapa mafunzo wanajeshi na maafisa wa polisi ili kufanikisha azma yao ya kuunda serikali ya kinzani. Serikali ya Kongo imezifunga benki na kusitisha huduma nyingine za msingi baada ya wafanyakazi wa umma kukimbia Mashariki mwa Kongo kutokana na mapigano.

Kwa mujibu wa kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Corneille Nangaa azma yao ni kuipindua serikali ya Rais Felix Tshisekedi na kuunda uongozi mpya unaojikita katika uwazi na utendaji.

Kibarua chao kikubwa ni kuwabadili wakaazi mawazo na kuwarai kuwa na imani nao. Katika miezi ya kwanza, M23 iliteua magavana, madiwani, waratibu na kuanza kutoa huduma za vitambulisho na hati za usajili.

Vijana Goma waanzisha kumbukumbu ya matukio ya uhalifu

Miji ya Goma na Bukavu bado haina utulivu

Hata hivyo, miji mikubwa ya Goma na Bukavu ya majimbo ya Kivu ya Kaskazini na Kusini, haijakuwa na maafisa wa polisi wala mahakama zinazofanya kazi na hivyo kuwepo kwa ongezeko la visa vya uhalifu wanasema mashuhuda. Kufungwa kwa benki na mifumo ya biashara pia vimevuruga uchumi ambao tayari umedorora.

Duru zinaeleza kuwa tangu Agosti mwaka huu, M23 wametangaza mabadiliko kadhaa na kuchapisha video inayowaonyesha kikosi cha maafisa wake wapya wa polisi kilichojumuisha maafisa wa serikali wa zamani waliokamatwa wakati wa mashambulizi na wengine wapya.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Goma 2025 | Uongozi wa M23 katika mkutano na waandishi wa habari katikati ya mapigano
Kiongozi wa M23 Corneille Nangaa, Rais wa M23 Bertrand Bisimwa, Katibu Mkuu wa M23 Benjamin Mponimpa na mwanachama wa M23 Derio Kimbulungu kwenye mkutano na waandishi wa habari katika hoteli moja mjini Goma Januari 30, 2025. Picha: Cyrile Ndegeya/Anadolu/picture alliance

Haijabainika iwapo walijiunga kwa hiari au kushinikizwa. Lengo la video hiyo ni kuusisitizia umma kuwa wamejipanga na kuajiri wataalamu kinyume na hali ilivyo kwenye kikosi cha taifa ambacho kimechafuliwa na madai ya ufisadi. M23 pia imeandaa mtihani wa mchujo kwa ajili ya wanasheria wapatao 500 watakaowajumuishwa kwenye idara ya mahakama.

Kulingana na ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa ya Julai, kundi hilo limekuwa likiendesha operesheni zake za uongozi pasina vigezo vya msingi vya kisheria au mbinu za uwajibikaji hali inayozua adhabu na mauaji ya kiholela.

Ijapokuwa watuhumiwa wamefanyiwa msako ili kupunguza viwango vya uhalifu, mashirika ya kimataifa yanalalamika kuwa matokeo yake ni ukiukaji wa haki.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Mgodi wa dhahabu wa Luhihi-Goldmine katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Dhahabu ikisafishwa kwenye maabara ya Primera Gold huko Bukavu, Mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mei 12, 2023.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Suala la ufadhili kwa M23 bado kitendawili

Ufadhili wa kundi la M23 bado unazua hisia mseto kwani mfumo wa benki umeporomoka Kongo. Kwa mujibu wa Reagan Miviri, mtaalam wa utafiti katika taasisi ya Ebuteli ya Kongo, M23 inahitaji msaada wa kigeni kwani operesheni za kijeshi zinazoendelea zinahitaji ufadhili mkubwa.

Ili kufidia pengo hilo la benki M23 imeunda mamlaka ya fedha ya kukusanya mapato, kutenga kodi maalum za biashara na uchimbaji wa madini.

Hata hivyo wakaazi wanalalamika kuwa hawana chochote na wanashurutishwa kulipa kodi katika mazingira magumu ya vita Mwezi uliopita, chama kikuu cha wafanyakazi jimboni Kivu ya Kusini kiliwasilisha ujumbe kwa M23 kuwaomba wapate msamaha wa kodi kwani wanasakamwa na madhila ya vita.