1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

Myanmar yaomba kuungwa mkono na jamii ya kimataifa

Lilian Mtono
27 Machi 2023

Utawala wa kijeshi wa nchini Myanmar umewatolea mwito wakosoaji wake wa nje kuunga mkono mkakati wa utawala huo wa kurejea kwenye demokrasia.

https://p.dw.com/p/4PJr8
Myanmar | Militärparade in Naypyitaw
Picha: AFP/Getty Images

Utawala wa kijeshi wa nchini Myanmar aidha umewataka mataifa ya nje kuacha kuungana na vuguvugu linaloupinga utawala huo ambalo inauita "ugaidi" unaolenga kulivuruga taifa hilo.

Akihutubia katika siku ya gwaride la mwaka la majeshi ya taifa hilo, Min Haung Hlaing ambaye mapinduzi aliyoyaongoza ya mwaka 2021 yamelitumbukiza taifa hilo katika mgogoro mkubwa, amesema shutuma za kimataifa dhidi ya serikali yake ya kijeshi zilitokana na nadharia za uwongo za Serikali kivuli ya Umoja wa kitaifa, NUG.

Amesema serikali yake itafanya uchaguzi ifikapo mwezi Agosti ambao hata hivyo tayari unakosolewa kwa kiasi kikubwa, huku kukiwa na uwezekano wa baadhi ya vyama kuzuiwa kushiriki.

"Jeshi na serikali tunataka kuchukua hatua kali dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo yanajaribu kuivuruga nchi na kuwaua watu," amesema Ming Aung Hlaing. "Ningependa jumuiya ya kimataifa waunge mkono juhudi za serikali ya sasa kuelekea kwenye njia sasa ya demokrasia."

Soma Zaidi: Mtawala wa kijeshi wa Myanmar asema uchaguzi sharti ufanywe

Mapinduzi aliyoyaongoza yalihitimisha ghafla muongo wa demokrasia na hatua ambazo hazikuwa zimetarajiwa za maendeleo zilizokuwa zimepigwa nchini Myanmar.

Bangladesch Cox's Bazar  Flüchtlingslager
Mmoja ya wakimbizi wa Rohingya waliokimbia machafuko nchini Myanmar akiwa katika kambi ya Cox Bazaar nchini BangladeshPicha: Guven Yilmaz /AA/picture alliance

Waislamu wengi wa Myanmar wanaendelea kukimbia makambi ya wakimbizi, Bangladesh.

Kando na hotuba hiyo, taarifa nyingine zinasema zaidi ya Waislamu wa Rohingya 180 wamewasili katika jimbo la Aceh nchini Indonesia mapema hii leo.

Mkuu wa polisi wa Aceh Mashariki Andy Rahmansyah amesema "Taarifa tulizozipata zinasema nahodha wa boti iliyokuwa imewabeba aliwaacha ufukweni na kuwaambia tayari wamefika mahali walipokuwa wakielekea." Amesema polisi wanaendelea kukusanya taarifa na wengine wanapatiwa huduma za matibabu.

Ali Hussein, mmoja ya wakimbizi hao wa Rohingya amesema boti hiyo iliwachukua Banlgadesh kabla ya kuwatelekeza gizani. "Hali ilikuwa ngumu sana kule. Tulipokuwa tumekusanyika tulipata hiyo fursa ya kuondoka na boti na tulikubali kwenda mbali kabisa, iwe Indonesia ama Malaysia," alisema Hussein.

Zaidi ya Warohingya 700,000 kutoka madhehebu ya Waislamu walio wengi ya Buddha nchini Myanmar walikimbilia katika makambi ya wakimbizi ya Bangladesh baada ya jeshi kuanzisha hatua kali mwezi Agosti, 2017. Vikosi vya usalama vya Myanmar vimekuwa vikituhumiwa kwa mauaji, ubakaji wa watu wengi na kuchoma maelfu ya makazi ya Warohingya.

Wengi wa wakimbizi hao hata hivyo wamejaribu kukimbia kutoka kwenye makambi hayo na kwenda Malaysia ambako kunakaliwa na Waislamu wengi, ingawa waliishia Indonesia.