Mwinyi wa kwanza kuchukuwa fomu ya ZEC kuwania urais Zanzibar | Matukio ya Afrika | DW | 26.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

UCHAGUZI 2020

Mwinyi wa kwanza kuchukuwa fomu ya ZEC kuwania urais Zanzibar

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeanza kutoa fomu za kugombea urais wa visiwa hivyo yakiwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, huku mgombea wa chama tawala (CCM), Hussein Mwinyi, akiwa wa kwanza kujitokeza.

Wakati Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) ikifunga milango yake siku ya Jumanne (Agosti 25) kutowa na kurejesha fomu za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ubunge na udiwani, kwa upande wa Zanzibar zoezi lilianza siku ya Jumatano (Agosti 26) na lilitarajiwa kuendelea hadi Septemba 9.

Mgombea wa kwanza kuwasili kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) asubuhi ya Jumatano alikuwa Hussein Mwinyi wa chama tawala cha Mapinduzi (CCM), ambaye alifuatiwa na mwenzake wa chama cha Wakulima (AFP), Said Soud. 

Mwinyi anahudumu sasa kama waziri wa ulinzi katika serikali ya Tanzania, wakati Soud akiwa waziri asiye wizara maalum kwenye serikali ya Zanzibar. 

Akitoa fomu hizo na kueleza masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea hao, Mwenyekiti wa ZEC Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud alisema wagombea hao sasa walikuwa na dhima ya kusaka wadhamini na kurejesha fomu hizo baadaye kwa uhakiki.

Wakati mgombea Soud wa AFP aliondoka na gari lake kwenye ofisi za tume hiyo na kuelekea nyumbani kimya kimya kama masharti ya tume hiyo yalivyowekwa, Mwinyi wa CCM alielekea Kisiwandui kwenye ofisi za chama chake na kupokelewa kwa shamrashamra na burudani mbalimbali, na baadaye kutoa hotuba fupi kwa wafuasi wake.

Hata hivyo, mpinzani mkubwa wa mgombea wa CCM katika kiti cha urais wa Zanzibar ni mwanasiasa maarufu, Maalim Seif Sharif Hamad, anayegombea kwa mara ya sita mfululizo.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye mara hii anawania kupitia chama chake kipya cha ACT Wazalendo, kwa sasa yupo nchini Dubai kwa mapumziko na anatarajiwa kurudi Zanzibar mwishoni mwa wiki.

Ripoti ya Salma Said/DW Zanzibar