Mwili wa Tshisekedi warejeshwa DRC | NRS-Import | DW | 31.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Mwili wa Tshisekedi warejeshwa DRC

Wakaazi mjini Kinshasa walijitokeza kwa wingi kuupokea mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi uliorejeshwa jana nchini DRC kwa ajili ya mazishi ya kitaifa hapo kesho Jumamosi.

Kuwasili kwa mwili wa Etienne Tsisekedi kulizusha majonzi na huzuni kubwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye uwanja wa ndege. Mwanae na ambae pia ni rais wa sasa Felix Tshisekedi pamoja na mkewe, maafisa wa serikali na viongozi wa kidini, walikuwa mstari wa mbele kuupokea mwili huo uliowekwa kwenye jeneza jeupe na kufunikwa na bendera ya kitaifa ya Kongo. Heshima za kijeshi na gwaride la polisi zilitolewa kutokana na kwamba Etienne Tshisekedi alikuwa waziri mkuu wa zamani 

 Mjane wa Etienne Tshisekedi, Marthe Kasalu pia alirejea na mwili wa mume wake kwenye ndege maalumu iliyokodishwa nchini Ubeljiji. Msafara mrefu wa magari na mamia ya maelfu ya wafuasi wa Tshisekedi waliusindikiza mwili huo hadi katikakati mwa mji huo kwa zaidi ya muda wa saa 7. Katika safari yake hiyo ya mwisho, mwili wa Tshisekedi uliwekwa zaidi ya saa moja kwenye makao makuu ya chama chake cha UDPS ambako umati wa watu ulikuwa ukiusubiri. Lisanga Bonganga ambae alikuwa rafiki wa Tshisekedi amesema kwamba shujaa haliliwi bali hushangiliwa .

Mamia ya waombolezaji waulaki mwili wa Tshisekedi mjini Kinshasa

Mamia ya waombolezaji waulaki mwili wa Tshisekedi mjini Kinshasa

Wafuasi wake walikesha kwenye makao makuu ya UDPS mtaani Limete huku wakiwasha mishumaa kama alama ya maombolezo.

Mwili wa Etienne Tshisekedi ulitarajiwa kuwasili Alhamisi asubuhi, lakini kutokana na matatizo ya mandalizi uliahirishwa hadi usiku. Kamati ya maandalizi ya mazishi inasema kwamba mipangilio ya awali haitobadilika. Leo Ijumaa itakuwa ni maombolezi ya kitaifa na hapo kesho itakuwa ni sala na ibada ya wafu kabla ya mazishi jioni. Urithi wa Tshisekedi umeelezewa na wafuasi wake kuwa vita vyake kwa ajili ya demokrasia.

Marais sita walihakikisha kuhudhuria mazishi hayo, huku swali kubwa leo kwa wakaazi wa Kinshasa ni kufahamu ikiwa rais  mstaafu Joseph Kabila atahudhuria au hapana. Baada ya miaka 18 ya uongozi wake, kabila na Tshisekei hawakuwahi kuonana ana kwa ana. 

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com