Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr anafikiria kujiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr anafikiria kujiuzulu

Idadi ya washirika wa Rais Donald Trump inaendelea kupungua wakati mwanasheria mkuu akiripotiwa kuwa anafikiria kujiuzulu akipingana na tabia ya Trump kuchapisha mtandaoni taarifa juu ya uchunguzi wa idara ya mahakama.

USA | William Barr

Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr akizungumza katika mkutano wa sheria mjini Washington.

Idara ya Mahakama nchini Marekani huenda ikapata pigo baada ya mwanasheria mkuu nchini humo kuripotiwa kuwaeleza watu wa karibu wa Trump kuhusu wasiwasi wake juu ya Tweet za Trump. Hata hivyo, haijabainika wazi iwapo mwanasheria huyo mkuu amemueleza Trump moja kwa moja juu ya nia yake, Gazeti la Washington Post limeripoti.

Gazeti hilo limemnukuu mtu mmoja aliye na ukaribu na Barr aliyesema kuwa Mwanasheria Mkuu huyo ana mipaka yake.

Gazeti hilo limeongeza kuwa Barr huenda anawaeleza watu wa karibu wa Rais Trump juu ya kadhia yake akiwa na lengo kuwa ujumbe wake utamfikia Trump ili awache kuandika hisia zake kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchunguzi wa idara ya mahakama.

Yamkini Ikulu ya White House na Idara ya mahakama haijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo la Mwanasheria mkuu kutafakari kujiuzulu licha ya ombi la Gazeti la Washington Post kutaka maoni kutoka kwao.

Msemaji wa Idara ya Mahakama azitaja kama porojo tetesi za Barr kujiuzulu 

USA | US-Justizminister fordert: Präsident Trump soll weniger twittern

Mwanasheria Mkuu William Barr akiwa na Rais Donald Trump mbele ya Ikulu

Hata hivyo, msemaji wa Idara ya Mahakama Kerri Kupec amepuzilia mbali tetesi hizo za Barr kuwa na nia ya kujiuzulu na kuzitaja kama porojo tu. Kupec ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa: "Mwanasheria Mkuu hana mpango wa kujizulu"

Haya yanajiri baada ya Trump kusema mnamo Jumanne kuwa ana imani na utendakazi wa Barr, ambaye wiki iliyopita alisema katika mahojiano kuwa tabia ya Trump ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa inatatiza kazi yake.

Trump naye alikiri mbele ya waandishi habari kuwa ni kweli anaifanya kazi ya Barr kuwa nguvu. Hata hivyo, alimsifu Mwanasheria mkuu huyo kwa kumtaja kuwa mtu mwenye uadilifu mkubwa.

Licha ya Barr kukerwa na tabia ya Trump ya kutumia mitandao ya kijamii, Rais huyo wa Marekani anaonekana kupuuza wito wa kumtaka akomeshe tabia hiyo kwa kusema anahisi mitandao ya kijamii ni muhimu kwani imempa nafasi ya kuwa na sauti.

Wiki iliyopita maafisa katika idara ya mahakama walimuondolea hukumu rafiki wa karibu wa Trump, Roger Stone, aliyepatikana na hatia ya kulidanganya bunge la Congress mnamo mwezi Novemba. Hatua ya maafisa hao ilizua tafrani katika idara hiyo. Kilichofuata ni shinikizo za kumtaka Barr kujiuzulu.

Trump alitumia mtandao wa Twitter kuwashambulia waendesha mashtaka wanne pamoja na jaji ambao walikuwa wanaiskiliza kesi ya Stone.

 

Vyanzo: DPA/AP/Reuters