1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiZimbabwe

Mwanaharakati wa Zimbabwe apewa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika

27 Novemba 2025

Jopo huru la majaji 20 limemtunukia Namatai Kwekweza, Tuzo ya Ujerumani kwa bara la Afrika kwa mwaka huu wa 2025 kwa kujitolea kwake kwa ujasiri kupigania utawala bora wa sheria na demokrasia nchini mwake Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/54NbM
Deutschland Berlin 2025 | Preisverleihung des Deutschen Afrikapreises an Namatai Kwekweza
Picha: Luisa von Richthofen/DW

 

Mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 26 raia wa Zimbabwe, Namatai Kwekweza mshindi wa mwaka huu wa Tuzo ya Afrika inayotolewa na Ujerumani alipokea Tuzo hiyo mbele ya hadhira teule iliyokusanyika mjini Berlin siku ya Jumatano.

Jopo huru la wanachama 20 limesema harakati za Kwekweza zinatoa ujumbe mkubwa wa kujiamini kuelekea kuifufua demokrasia. Binti huyo aliibuka kidedea kutoka kwa zaidi ya wateule 28 waliofanikiwa kuingia kwenye kinyang'anyiro cha mwisho cha kumsaka mshindi.

Katika hotuba yake kwenye sherehe hiyo, Rais wa Bunge la Ujerumani, Julia Klöckner alimsifu Kwekweza kwa kuchochea demokrasia na utawala wa sheria nchini mwake.

DW | 77 Asilimia | 2025 | Namatai Kwekweza
Akiwa na umri wa miaka 18, alianzisha shirika la kukuza vipaji vya vijana, leo Namatai Kwekweza (wa pili kutoka kushoto) amekuwa sehemu muhimu ya maisha ya umma nchini Zimbabwe.Picha: DW

Akiwa na umri wa miaka 18, Namatai Kwekweza alianzisha shirika la WELEAD Trust, linalowafunza viongozi vijana na linawashirikisha katika michakato ya kufanya maamuzi ya kisiasa.

Mwakilishi wa kizazi kipya

Alipoulizwa jinsi alivyojihisi baada ya kupokea tuzo hiyo ya heshima kubwa, Kwekweza aliisifu jamii yake na wenzake wa shirika la WELEAD Africa ambao amesema ndio nguvu kubwa iliyo nyuma yake.

Kwekweza amesema tuzo yake ni kwa ajili ya vijana wote wanaosimama imara na wanaolipa gharama kubwa kwa kutetea demokrasia.

Katika hali ya ukandamizaji inayozidi kuongezeka nchini Zimbabwe, Kwekweza anapigania utawala wa sheria na ushiriki sawa wa kisiasa. Amejihatarisha kwingi kwa ajili ya hili: Amekamatwa mara kadhaa na ameripoti juu ya mateso na vitisho dhidi yake lakini amesema havunjiki moyo kwa sababu kila mafanikio yana gharama yake.

Mwenyekiti wa baraza la majaji kwenye Jopo huru, Claus Stäcker, ambaye ni Mkurugenzi wa Idhaa za Afrika za Deutsche Welle, ameelezea kwamba kasi ya hivi karibuni katika uanaharakati wa vijana barani Afrika imechochea maamuzi ya baraza hilo la majaji.

"Kote barani Afrika, vijana wamejitolea kushiriki, kuhakikisha uwazi, na mabadiliko ya kijamii, kama vile harakati za hivi karibuni za maandamano ya Kizazi cha GenZ nchini Kenya, Madagasca, Cameroon na Tanzania, zinavyoonyesha. Na binti huyi Namatai Kwekweza ni mfano mkubwa wa kizazi hicho kipya cha wanademokrasia ambao sio tu wanapinga jambo fulani bali kwa ujasiri wanachukua majukumu ambayo yanaunda mustakabali wa nchi zao."

Claus Stäcker
Mwenyekiti wa baraza la majaji kwenye Jopo huru, Claus Stäcker, ambaye ni Mkurugenzi wa Idhaa za Afrika za Deutsche Welle

Majaji wa Jopo huru la Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika, Namatai Kwekweza, ni mfano wa kuigwa na kizazi kipya cha wanademokrasia, wanaochukua majukumu kwa ujasiri na hivyo kusaidia kujenga mustakabali mzuri wa nchi zao.

Tuzo hiyo ni utambuzi wa juu zaidi wa Wajerumani kwa Waafrika. Inatolewa na Wakfu wa German Africa - wakfu usioegemea upande wowote uliojitolea kukuza taswira bora bora ya bara la Afrika kwenye uwanja wa kisiasa miongoni mwa umma wa Wajerumani.

Tangu mwaka 1993, imewatunukia Tuzo hiyo watu kutoka bara la Afrika ambao wametoa mchango wa kipekee kwa demokrasia, amani, haki za binadamu, maendeleo endelevu, utafiti, sanaa, utamaduni, na pia masuala ya kijamii barani Afrika.

Yvonne Aki Sawyerr
Kushoto: Yvonne Aki-Sawyerr, mshindi wa Tuzo Ujerumani kwa Afrika mwaka 2024Picha: Luisa von Richthofen/DW

Mwaka jana, Meya wa mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, Yvonne Aki-Sawyerr, alipokea tuzo hiyo. Wapokeaji wengine ni pamoja na watafiti wa COVID, Tulio de Oliveira na Sikhulile Moyo, Rais wa zamani wa Botswana Ketumile Masire na wanaharakati wa Somalia Waris Dirie na Ilwad Elman.