Mwaka wa maafa zaidi kwa waandishi wa habari | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mwaka wa maafa zaidi kwa waandishi wa habari

Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka limesema mwaka huu wa 2012 ndiyo ulikuwa wa maafa zaidi kwa waandishi wa habari ulimwenguni. Limeyasema hayo katika ripoti yake ya mwaka iliyotolewa tarehe 19.12.2012.

Uhuru wa waandishi wa habari.

Uhuru wa waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waandishi wa habari 88 waliuawa wakati wakiripoti kutoka maeneo yenye vita na mashambulizi ya mabomu, au waliuawa na makundi ya uhalifu na wasafirishaji wa dawa za kulevya, au kwa amri za wapiganaji wa kiislamu na maafisa wala rushwa.

Mwandishi wa habari wa Urusi Kazbek Gekkiev ni moja wa waliyouawa mwaka huu.

Mwandishi wa habari wa Urusi Kazbek Gekkiev ni moja wa waliyouawa mwaka huu.

"Mwaka 2012 waandishi wa habari wengi zaidi wamepoteza maisha yao kuliko ilivyowahi kutokea tangu kuanza kutolewa kwa ripoti ya kila mwaka ya shirika la waandishi wa habari wasiyo na mipaka mwaka 1995," amesema Ulrike Gruska, Afisa kutoka shirika la wandishi wa habari wasiyo na mipaka.

Hali ya waandishi habari nchini Syria

Mwaka huu ulikuwa mbaya hasa kwa waandishi wa kiria, maarufu kama Citizens Journalists, wana blogi na waandishi wa habari za kwenye mtandao. Mwaka uliyopita ni waandishi watano waliouawa, mwaka huu idadi imepanda hadi kufikia 47, huku 44 kati yao wakiwa wameuawa nchini Syria.

"Nchini Syria wengi wameuawa wakati wakijaribu kuvunja vizuizi vya upatikanaji wa habari vilivyowekwa na utawala wa nchi hiyo, kwa kujaribu kupeleka taarifa nje ya mipaka ya nchi hiyo kwa njia ya ujumba wa blogi, video au hata ujumbe wa simu za mkononi," anongeza Gruska.

Mhariri wa jarida la Orient Nils Metzger anasema tatizo linalowakumba waandishi wa habari nchini Syria ni kuzingirwa katika mapigano, na pande zote zinazohusika katika mgogoro huo zimeshiriki kuua wandishi wa habari. Anasema waasi kwa mfano hawachukulii waandishi wa vyombo vya serikali kama waandishi wasiyoegemea upande katika mgogoro huo na wamekuwa wakiwauwa.

Mwandishi wa habari wa Marekani Marie Colvin aliuawa nchini Syria mwaka huu.

Mwandishi wa habari wa Marekani Marie Colvin aliuawa nchini Syria mwaka huu.

Metzger anasema hata wafanyakazi wa mashirika ya habari ya Urusi wako katika hatari kubwa. Anatoa mfano pia wa uripuaji wa kituo cha habari cha upinzani na vikosi vya serikali. Jumla ya wandihi wa habari 65 wameuawa nchini Syria mwaka huu wakati wanatekeleza majukumu yao, huku 21 wakiswekwa rumande.

Mwaka mbaya zaidi kwa tasnia ya habari nchini Somalia

Ripoti hiyo inasema mwaka huu wa 2012 umekuwa mwaka mweusi kwa sekta ya habari nchini Somalia, ambako waandishi 18 wameuawa. Nchini Pakistan wandishi wa habari 10 wameuawa.

Nchini Mexico, ripoti hiyo inasema waandishi wanaishi maisha ya hatari, hasa wanapokuwa wanaripoti kuhusu uhalifu, usafirishaji wa dawa za kulevya, na uhusiano kati ya viongozi wa magenge ya wahalifu na wafanyakazi wa umma. Waandishi sita wameuawa nchini Mexico mwaka huu. Shirika hilo linaiangazia pia Brazil kama mojawapo ya nchi hatari kwa waandishi wa habari ambapo wandishi watano wameuawa vibaya kwa sababu walikuwa wanachunguza biashara ya dawa za kulevya.

Kamata kamata, vitisho vyaendelea

Jambo lingine linalotia wasi wasi, ni idadi kubwa ya waandishi waliyofungwa jela mwaka huu. Ripoti hiyo inasema zaidi ya waandishi wa habari na wana blogi 1000 walikamatwa mwaka huu, huku wengine zaidi ya 2000 wakipewa vitisho.

Waandamanaji wakitaka kuachiwa kwa waandishi wa habari waliyokuwa wamefungwa nchini Afghanistan.

Waandamanaji wakitaka kuachiwa kwa waandishi wa habari waliyokuwa wamefungwa nchini Afghanistan.

Mpaka sasa hivi wandishi 193 wako jella, 70 kati yao wakiwa nchini Uturuki na Shirika linasema 42 kati yao wako ndani kwa sababu zinazohusiana na kazi yao. China pia imeripotiwa kuwafunga waandishi wa habari, na hadi wakati huu kuna waandishi wapatao 100 katika jela za China, huku wakiripotiwa kuishi katika mazingira mabaya.

Eritrea bado yaongoza kuwatesa waandishi Afrika

Katika kanda ya Afrika mashariki, Eritrea imeelezwa kuwa ndiyo nchi inayoongozwa kwa unyanyasaji wa waandishi wa habari. Hivi sasa kuna waandishi 28 katika jela za nchi hiyo, wengi wao wakiwa wakiwa wamewekwa katika jela za chini ya ardhi na kuachwa kuozea huko. nchini nyingine zilizotajwa kuendeleza unyanyasaji mkubwa wa waandishi wa habari ni pamoja na Oman, Cuba, Iran, Mali. Lakini ripoti haikutaja hali katika nchi za Magharibi.

Mwandishi: Heinze Henrik/Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com