Mursi awa ngangari | Matukio ya Afrika | DW | 27.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mursi awa ngangari

Rais wa Misri, Mohammed Mursi, amewaambia wapinzani wake watumie uchaguzi na siyo maandamano kubadilisha serikali, na kusema kuwa jeshi linapaswa kujikita katika jukumu lake la ulinzi wa taifa.

Mursi na Abdel-Fattah

Mursi na Abdel-Fattah

Matamshi ya rais Mursi kwa jeshi la Misri yamekuja huku wapinzani wakiwa na matumaini kuwa majenerali wa jeshi hilo wenye nguvu watalinda maandamano yao siku ya Jumapili katika kuonyesha kuwaunga mkono. Akizungumza katika ukumbi mkubwa uliojaa watu, Mursi alikumbusha kuwa wote wanakubaliana kuwa rais ndiye Amiri Jeshi mkuu, na kuongeza kuwa wapo wasiotaka kuona rais na jeshi wakiwa na uhusiano mzuri.

Wafuasi wa rais Musri wakiandamana kuonyesha mshikamano hivi karibuni.

Wafuasi wa rais Musri wakiandamana kuonyesha mshikamano hivi karibuni.

Hadhira hiyo iliyojumuisha mawaziri, maafisa kutoka chama cha rais Mursi cha Udugu wa Kiislamu na wafuasi wengine, ilishangilia matamshi yake kuhusu jeshi, ambayo wakati mwingine yalionekana kama kejeli kwa waziri wa ulinzi Abdel-Fattah el-Sissi, ambae alikuwa amekaa kimya katika msitari wa mbele. El-Sissi alitoa kauli nzito huko nyuma akizitaka pande mbili zifanye suluhu, na kuonya kuwa jeshi lisingekaa kimya wakati tofauti za kisiasa zikihatarisha utengamano wa taifa.

Akiri kufanya makosa

Mapema siku ya Jumatano, maafisa wa jeshi walisema wanaimarisha ulinzi katika miji mikubwa ya Misri, kwa tahadhari iwapo vurugu zitatokea siku ya Jumapili. Katika hotuba yake iliyodumu saa mbili na nusu, Mursi alitetea utendaji wake katika mwaka wake wa kwanza ofisini, akikiri kufanya makosa lakini pia akidai kuwa na mafanikio. Wakati mmoja aliomba radhi kutokana na uhaba wa mafuta, na wakati mwingine aliwaomba radhi vijana wa taifa hilo kwa kutowashirikisha vya kutosha katika mfumo wa kisiasa wa Misri, na kuwaagiza mawaziri na magavana kuwateua wasaidizi walio na umri chini ya miaka 40.

"Nimefanya makosa mengi na wakati huo nimepata mafanikio mengi, huu ndiyo ukweli. Maendeleo ya kiuchumi yemcheleweshwa na inabidi kuongeze bidii katika hili, na hii inahitaji suluhusu ya kiasiasa na utulivu. Katika mwaka uliopita nimegundua kuwa ili mapinduzi yatimize shabaha na malengo yake, laazima kuwepo na mageuzi makubwa katika taasisi za nchi," alisema.

Hotuba yake imekuja siku chache kabla ya maandamano yaliyopangwa na upinzani kwa lengo la kumuondoa madarakani. Lakini Mursi hatukoa tahfif katika mgogoro unaoendelea kati yake na wapinzani hao, na badala yake aliwaambia washiriki uchaguzi kama wanataka kumuondoa madarakani.

Rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kihali nchini Misri aliwashtumu wapinzani kwa kukataa wito wake wa kufanya majadiliano kuhusu matatizo yanayolikumba taifa. Pia alivitaka vyombo vya habari kuacha kusambaza habari za uongo na kuchochea chuki. Aliiambia mahakama, ambayo amekuwa akikwaruzana nayo mara kwa mara, kujiepusha na siasa, ingawa aliongeza kuwa anaheshimu sana hadhi yao.

Waandamanaji wanaompinga rais Mursi.

Waandamanaji wanaompinga rais Mursi.

Mikono salama zaidi kwa Misri

Wapinzani wanataka kumuondoa Mursi madarakani kwa madai kuwa ameshindwa kuiendesha vizuri nchi, kutokana na kufanya maamuzi ya upande mmoja, na kwamba ameingilia uhuru wa mahakama, na hivyo wameandaa maandamano makubwa siku ya Jumapili, kujaribu kumshinikiza aitishe uchaguzi wa mapema, jambo ambalo mwenyewe amesema linakwenda kinyume na demokrasia.

Kwa ujumla hotuba ya Mursi ililenga kumuonyesha mikono salama zaidi kwa taifa hilo katika wakati mgumu, jambo alilojaribu kuwasilisha kwa kuzungumzia njama za nje kuivuruga Misri, na maafisa watiifu kwa Hosni Mubarak kujaribu kuivuruga serikali yake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,dpae
Mhariri: Josephat Charo