Mursi arejea Ikulu baada ya kutimuliwa na maandamano | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mursi arejea Ikulu baada ya kutimuliwa na maandamano

Rais Mohammed Mursi wa Misri amerejea kazini asubuhi ya leo baada ya kulazimika kuondoka kutoka Ikulu jana jioni kuepuka waandamanaji walioizingira ofisi yake. Maandamano hayo ni kupinga uamuzi wake kujiongezea madaraka.

Maandamano Cairo

Maandamano Cairo

Mamia ya waandamanaji wanaosalia mbele ya ofisi za Rais Mursi ni mabaki ya maelfu waliojitokeza jana jioni, kuizingira ofisi ya rais huyo na kupaza sauti wakimtaka aondoke. Wale walioamua kubaki wanadai hawaondoki hadi pale Mursi atakapoondosha kanuni aliyoiweka ya kujilimbikizia madaraka.

Waandamanaji hao, kama mmoja wao anavyodai, wanasema wanapigania uhuru wao na hawamuamini tena rais Mursi kuuhakikisha uhuru huo. ''Hatuwezi tena kuzungumza kwa uhuru, na hakutakuwa na mahakama zinazofanya kazi kwa uhuru. Mursi anasema hatabakia madarakani milele, lakini hatumuamini. Haya tumeyazoea, tumetawaliwa na Mubarak miaka 30. Mursi hatajitolea kuachia madaraka. Hilo tunalijua bayana''. Alisema mwandamanaji huyo.

Mohammed Mursi wa Misri. Uamuzi wake kujilimbikizia madaraka umeligawa taifa

Mohammed Mursi wa Misri. Uamuzi wake kujilimbikizia madaraka umeligawa taifa

Hata hivyo, hali imeanza kuwa ya kawaida. Kabla ya mapambazuko leo, wachuuzi walikuwa wameanza kupanga bidhaa zao kwenye ukuta wa Ikulu ya Itihadiya, ambao umechafuliwa kwa maandishi na michoro ya graffiti, yenye ujumbe unaompinga Rais Mursi.

Ni kwa nini rais Mursi ameamua hivyo? Aliuliza mmoja wa waandamanaji waliokwenda Ikulu na kuongeza kuwa kwa maoni yake, Mursi anapaswa kuwa rais wa wamisri wote, na siyo wa kundi la Udugu wa Kiislamu.

Magazeti nayo hayakubaki nyuma katika kumshambulia rais huyo wa Misri. ''Onyo la mwisho, Ikulu imezingirwa,'' ndicho kilichokuwa kichwa cha habari kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la kila siku al-Shuruk. Nalo gazeti la binafsi la al-Watan lilikuwa na kichwa cha habari kinachosema: ''Mapinduzi kwenye mlango wa Ikulu.''

Michoro inayomkosoa rais Mursi kwenye kuta mjini Cairo

Michoro inayomkosoa rais Mursi kwenye kuta mjini Cairo

Mamia ya waandamanaji wengine wamekusanyika katika viwanja maarufu vya Tahrir, wakijihifadhi katika mahema yaliyojengwa takribani wiki mbili zilizopita. Wanaharakati walitumia mitandao ya kijamii kuwataka watu wawapelekee waandamanaji chakula na blanketi.

Maandamanao hayo ya jana, ambayo polisi ilijaribu kuyatawanya kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozi, yaliashiria mpasuko zaidi baina ya kambi kadhaa zenye maoni yanayotofautiana nchini Misri.

Maandamano hayo yalikuwa hatua nyingine dhidi ya uamuzi uliochukuliwa na Rais Mursi tarehe 22 Novemba kujiongezea madaraka, na ambao ulimwezesha kuitisha kura ya maoni katikati mwa mwezi huu wa Desemba, kuhusu rasimu ya katiba ambayo iliandikwa na jopo linalodhibitiwa na wajumbe kutoka vyama vya Kiislamu.

Rasimu hiyo inapingwa na Waliberali, Wakristo na pia wanasiasa wa mrengo wa kushoto, wakisema kwamba inaigeuza Misri kuwa nchi ya kidini. Makundi hayo hayataki mambo ya dini kuingizwa kwenye siasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com