1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpasuko wanukia katika chama cha Jubilee

Shisia Wasilwa 10 Septemba 2019

Wabunge wanaoegemea upande wa naibu rais wa Kenya William Ruto, wanamtaka rais Uhuru Kenyatta kujitokeza wazi na kuelezea jinsi wanavyodhulumiwa na vyombo vya dola.

https://p.dw.com/p/3PKtW
Kenias Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: picture-alliance/B.Inganga

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mbunge mmoja kutiwa nguvuni kwa kutatiza hafla ya mchango kanisani katika jimbo lake la uchaguzi analoliwakilisha bungeni. Wabunge hao wanadai kuwa hizo ni njama za kuwanyamazisha wasiiunge mkono azma ya Ruto kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kimya cha rais Kenyatta kuhusu matukio yanayokizonga chama tawala cha Jubilee kinatishia kukipasua na kukisambaratisha hata zaidi, huku salamu za heri kati yake na kinara wa upinzani Raila Odinga zikileta shari na miumano chamani badala ya umoja.

Kutiwa nguvuni kwa mbunge wa Jubilee Ndindi Njoro, baada ya kuvamia hafla ya mchango wa pesa kanisani, uliokuwa ukiongozwa na kundi la Kieleweke Jumapili, kumeongeza mianya kwenye chama hicho ambacho wadadisi wa siasa wanasema hakitaishi kuona uchaguzi mwingine mkuu, iwapo misuguano itaendelea kushuhudiwa.

Mpasuko wa chama hicho unashuhudiwa sana katika ngome ya kisiasa ya rais Uhuru ya Mlima Kenya ambapo pameibuka makundi mawili ya Tangatanga na Kieleweke. Njoro anaegemea upande wa Kieleweke unaomuuunga mkono naibu rais William Ruto.

Wabunge wamtaka rais Kenyatta kueleza wazi ni upande upi anaouunga mkono

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Rasi wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu rais wake William RutoPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Viongozi hao wanaonya kuwa, kimya cha rais kinathibitisha kuwa ameagiza vyombo vya dola kuwanyamazisha na kuwatisha wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto. Aidha wanataka rais aelezee msimamo wake kuhusu nani anayemuunga mkono kati ya Raila na Ruto.

Mbunge wa Kandara Alice Wahome amenukuliwa akidai kuwa baadhi ya wafanyibiashara wenye ushawishi kutoka eneo la Mlima Kenya wamekuwa wakifanya mikutano na vyombo vya dola kujadili jinsi ya kumzuia Ruto kumrithi rais Kenyatta.

Ndindi Nyoro amefikishwa mahakani hii leo na ameachiliwa bila ya kushtakiwa. Alipokamatwa huko Murang'a, ghasia zilishuhudiwa kwa muda kabla ya hali kurejea kawaida usiku wa kuamkia leo.

Mapema mwaka huu, wabunge wanaogemea upande wa Ruto wakiwemo gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa, wote kutoka eneo la Mlima Kenya walinyang'anywa walinzi wao kwa njia ya kutatanisha na kisha baadaye wakarejeshewa.

Chanzo: Dw Nairobi