1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Motsepe kuheshimu uamuzi wa CAS kuhusu Senegal

30 Machi 2026

Rais wa CAF Patrice Motsepe amesema atauheshimu uamuzi wa mahakama ya CAS kuhusu Senegal kuvuliwa ubingwa wa Afrika.

https://p.dw.com/p/5BOZb
Rais wa CAF Patrice Motsepe
Rais wa CAF Patrice MotsepePicha: Wu Tianyu/Xinhua/IMAGO

Senegal ilikata rufaa katika mahakama hiyo iliyo na makao yake mjini Geneva, Uswisi, baada ya tangazo la CAF kwamba mahakama yake ya rufaa imeupindua ushindi wa 1-0 wa Senegal dhidi ya Morocco mnamo mwezi Januari.

CAF ilidai kuwa vurugu zilizotokea kwenye fainalihiyo ziliipelekea kuipa ubingwa Morocco. Senegal ilikata rufaa na katika mechi ya kirafiki ya Jumamosi timu hiyo ilipocheza na Peru, iliwasilisha mbele ya mashabiki uwanjani kombe la AFCON kuashiria pingamizi lake kwa uamuzi wa CAF.

Senegal katika mechi hiyo ilicheza na fulana zilizo na nyota mbili kuashiria ubingwa wao mara mbili wa AFCON mara ya kwanza ikiwa 2022 na wa pili huo wa 2026 ulio na utata.

"Nitauheshimu na kuutekeleza uamuzi wa CAS. Maoni yangu kuhusiana na suala hilo hayana maana," alisema Motsepe akiwa mjini Cairo baada ya kukutana na maafisa wa CAF.

Kamati ya nidhamu ya CAF iliwaadhibu wachezaji na maafisa kadhaa kutoka timu zote mbili zilizoshiriki fainali Senegal na Morocco baada ya vurugu zilizoshuhudiwa uwanjani, ila kamati hiyo haikubadilisha matokeo.

Mashindano mengine ya AFCON yatafanyika Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu 1976 huku Kenya, Tanzania na Uganda wakitarajiwa kuwa waandalizi.