Mlipuko wa Ebola unasambaa kwa kasi zaidi Kongo
10 Julai 2026
Kufikia sasa, WHO imethibitisha visa 1,759 vyaEbola nchini DRC, vikiwemo vifo 600, huku wagonjwa 285 wakipona. Mlipuko huo umeenea katika majimbo manne, lakini unaathiri zaidi jimbo la Ituri.
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC, kinasema huu ndio mripuko wa Ebola unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kurekodiwa, ukiipita hata milipuko ya awali ya aina ya Bundibugyo na aina nyingine zote za virusi vya Ebola. Mkurugenzi wa Kituo cha Dharura za Afya wa Africa CDC, Dkt. Wessam Mankoula amesema kasi ya Ebola ni ya kutisha.
"Huu ndio mripuko wa Ebola unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa, si tu ukilinganishwa na milipuko ya awali ya Bundibugyo, bali pia ukilinganishwa na aina zote za virusi vinavyosababisha Ebola", alitahadharisha Mankoula.
Mankoula amesema katika wiki sita za kwanza pekee, mlipuko huu ulifikia zaidi ya visa 1,500, ikilinganishwa na visa 994 vya mlipuko mkubwa zaidi wa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2013 na 2016. Ameonya kuwa virusi vinaendelea kusambaa kwa kasi kuliko uwezo wa mamlaka za afya kupeleka rasilimali za kukabiliana navyo.
Majaribio ya chanjo dhidi ya Ebola
Africa CDC inasema takribani dola bilioni 1.4 zinahitajika ili kugharamia operesheni za afya na misaada ya kibinadamu, huku ikitoa wito kwa wafadhili kuharakisha utoaji wa fedha na wataalamu wa afya.
Mlipuko huu unasababishwa na aina adimu ya virusi vya Bundibugyo, ambayo hadi sasa haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa. WHOinasema takribani mtu mmoja kati ya watatu wanaoambukizwa hufariki dunia.
Wakati huo huo, majaribio ya dawa mbili zinazotarajiwa kutibu aina hiyo ya Ebola yameanza nchini DRC, huku yakichunguza ufanisi wa kingamwili ya MBP134 na dawa ya Remdesivir, peke yake na kwa pamoja.
Hata hivyo, WHO inaonya kuwa mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC, hususan katika jimbo la Kivu Kusini, pamoja na uhaba wa fedha za misaada, vinaendelea kutatiza juhudi za kudhibiti mlipuko huo. Aidha, zaidi ya watu 10,000 waliokutana na wagonjwa wanafuatiliwa, lakini kiwango cha ufuatiliaji bado kiko chini ya kiwango kinachohitajika ili kuukomesha mripuko huo.