Mkuu wa IMF atoa onyo kwa Marekani juu ya kubana matumizi. | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkuu wa IMF atoa onyo kwa Marekani juu ya kubana matumizi.

Mkuu wa shirika la kimataifa la fedha duniani Christine Lagarde ameonya juu ya mpango wa Marekani wa kubana matumizi usiwe mkali na wa lazima kwa kuwa huenda ukaathiri uchumi wa dunia nzima.

Mkuu wa IMF Christine Lagarde

Mkuu wa IMF Christine Lagarde

Katika mahojiano na shirika la habari la NBC Lagarde amesema Marekani inapaswa kujadili mpango wake wa kubana matumizi katika sekta za masuala ya jamii kama afya na usalama wa jamii na kusema kwamba haipaswi hata kidogo kwa Marekani kuweka hatua kali za kubana matumizi kwa kuwa huenda uchumi unaoanza kuinuka ukaporomoka tena.

Mkuu huyo wa IMF amesema jambo hili linapaswa kuangaliwa kwa makini ili kulinda ukuaji wa uchumi ambao kwa sasa unatoa nafasi za kazi na kusaidia kwa kila njia.

Christine Lagarde

Christine Lagarde

Christine Lagarde ameongeza kuwa ni jambo la msingi kwa serikali ya Marekani kufikia maelewano ya kufungua shughuli za serikali na kuendelea kukopa ili wasiweze kushindwa kulipa madeni yake.

Shughuli za baadhi ya ofisi za serikali ya Marekani zilifungwa tarehe mosi mwezi huu kufuatia bunge la nchi hiyo kushindwa kufikia makubaliano juu ya bajeti mpya.

Warepublikan ambao wanalidhibiti baraza la wawakilishi wanataka kucheleweshwa kwa mpango wa rais Obama wa kutoa huduma ya afya ujulikanao kama Obamacare. Wabunge hao wa Republican wanashinikiza sheria hiyo ya mabadiliko ya afya iondolewe au mpango huo hautapokea fedha za kuugharamia.

Marekani inakabiliwa na kitisho cha kutolipa madeni yake

Wakati huo huo Marekani inakabiliwa na kitisho cha kutoweza kulipa madeni yake baada ya wabunge warepublican na wale wa Demokrats kushindwa kukubaliana juu ya kufungwa huko kwa shughuli za serikali, na pia kuongeza kiwango cha ukopaji.

Bunge lilijaribu kuutatua mkwamo huo ulioingia siku yake ya 14 hii leo katika mkutano wake hapo jana jambo ambalo halikufua dafu na hali hii sasa imeliweka taifa hilo katika aibu kutokana na Marekani kuonekana kuwa nchi kubwa yenye nguvu na ilio na uchumi mkubwa duniani.

Jengo la Ikulu ya Marekani

Jengo la Ikulu ya Marekani

Iwapo kiwango cha ukopeshaji hakitopandishwa ifikapo Oktoba 17 basi huenda hazina ya serikali ikakosa pesa na kuanza kukumbwa na madeni kwa mara ya kwanza katika historia ya Marekani.

Kwa upande wake Mkuu wa Hazina ya Marekani Jacob Lew awali aliiambia kamati ya sera katika shirika la kimataifa la fedha kwamba Marekani inafahamu athari zilizopo.

Kwa sasa Masoko ya hisa yameingiwa na wasiwasi iwapo hakutakuwa na maafikiano kati ya chama cha Rais Barrack Obama cha demokrats na wenzao wa Republikan juu ya bajeti mpya na kiwango cha ukopaji ifikapo Alhamisi usiku.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com