1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Vatican wamalizika

Lilian Mtono
25 Februari 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amehitimisha mkutano usio wa kawaida uliojadili visa vya dhuluma za kingono dhidi ya watoto kwenye kanisa hilo. Aapa kukabiliana na wahusika kwa "ghadhabu ya Mungu". 

https://p.dw.com/p/3E2QO
Vatikan Missbrauchsgipfel Papat Franziskus
Picha: picture-alliance/S. Spaziani

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amehitimisha mkutano usio wa kawaida uliojadili visa vya dhuluma za kingono dhidi ya watoto vinavyofanywa na mapadre, huku akiapa kukabiliana na wahusika wa vitendo hivyo kwa kile alichokitaja kuwa ni "ghadhabu ya Mungu", lakini wakosoaji wakisema kuwa kiapo chake hicho hakitoshi kuchukuwa hatua stahiki kwa wahusika wa hivyo viovu. 

Hatua ya Papa Francis kushindwa kuja na mkakati madhubuti wa kuwatia hatiani mapadre na maaskofu wanaokutikana na makosa ya kushindwa kuwalinda watoto, imewaghadhabisha wahanga wa visa hivyo waliotarajia makubwa baada ya mkutano huo wa kwanza na wa aina yake kuwahi kufanyika katika kanisa hilo la Katoliki duniani.

Papa Francis alitoa hotuba yake mwishoni mwa ibada, mbele ya maaskofu wa Kikatoliki na wakuu wengine waandamizi wa madhehebu hayo walioitwa Roma, kufuatia kuongezeka kwa ripoti za visa vya unyanyasaji wa kingono, hali iliyotishia kuibuka kwa mzozo mkubwa kuhusu uaminifu wa viongozi hao na pia ndani ya utawala wa Papa Francis mwenyewe.

Vatikan-Missbrauchskonferenz Papst Franziskus
Papa Francis akiwa ibadani, wakati wa mkutano huo wa siku nne wa kujadili unyanyasaji wa kingono.Picha: AP

Ikiwa ni kama kiashiria cha kuanza kuchukuliwa kwa hatua, Vatican imeazimia kutangaza sheria mpya hivi karibuni itakayoweka sera ya kuwalinda watoto katika eneo la Vatican.

Hata hivyo, baadhi ya wahanga wa vitendo hivyo wameeleza kutoridhishwa na matamshi ya Papa kuhusu namna atakavyolishughulikia tatizo hilo, na wengine kufikia hatua ya kutaka kuwasilisha mashauri yao mahakamani.

Mark Rozzi, mbunge wa jimbo la Pennysylvania, aliyewahi kukabiliwa na unyanyasaji huo amesema "Kwenye hotuba yake, Papa amezungumzia kuhusu msamaha na kulipiza kisasi, nimeyapokea maneno yake. Lakini nilichokoina mimi ni kwamba alikuwa anawaambia maaskofu. Sawa, kwa upande wetu nadhani hii inamaanisha kwamba tunatakiwa kujua kwa nini haya yalitufika, na namna pekee tunayoweza kufanya ni kwenda mahakamani na kuwataja hadharani maaskofu ili kupata majibu yanayotufaa, yatakayotusaidia kuanza mchakato huu wa uponyaji." 

Menschen nehmen am "Marsch für Null Toleranz" in Rom teilÜberlebende des Sexmissbrauchs marschieren in Rom
Wahanga wa visa hivyo vya unyanyasaji, hawajaridhishwa na matamshi ya Papa kuhusu atakavyoshughulikia wahusikaPicha: picture-alliance/M. Spatari

Shirika la habari la Associated Press liliripoti mwaka jana kwamba makao makuu ya kanisa hilo la Kikatoliki hayakuwa na sera kama hiyo, ingawa lilisisitiza mnamo mwaka 2011 kwamba, makanisa yake yana sera hiyo. Miaka mitano iliyopita, liliuambia pia Umoja wa Mataifa kwamba sera kama hiyo kwa ajili ya Vatican ilikuwa inafanyiwa kazi. 

Kwenye hotuba yake ya mwisho baada ya mkutano huo wa kilele, Papa Francis amesisitiza kwamba matukio mengi ya unyanyasaji wa kingono yanatokea majumbani, hivyo kutaka suala hilo kutazamwa kwa mapana zaidi kuanzia kwenye jamii hadi picha za ngono zinazotazamwa mitandaoni, kama jaribio la kukabiliana na visa hivyo.

Mkutano huo wa kilele wa siku nne na uliomalizika jana uliwahusisha maaskofu kutoka kote duniani kwa lengo la kujadili visa vya ngono vinavyofanywa na viongozi hao dhidi ya watoto ndani ya kanisa hilo, suala ambalo si kitisho tu kwa mataifa, lakini pia linatishia lengo maalumu la kanisa hilo la Kikatoliki.

Amelitaka kanisa hilo kubadilika ili kusonga mbele, lakini pia akitaka vitendo hivyo kusemwa hadharani badala ya kuendelea kufunikwa kama ilivyo sasa.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef