1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Rais Joe Biden kwa mara nyingine amkosoa Netanyahu

Lilian Mtono
10 Machi 2024

Rais wa Marekani Joe Biden kwa mara nyingine ametoa matamshi makali dhidi ya operesheni za kijeshi za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4dM9m
Rais wa Marekani Joe Biden akitoa hotuba ya Hali ya Taifa
Rais Joe Biden akitoa hotuba ya Hali ya Taifa mbele ya bunge la Marekani ambapo alitoa wito kwa Israel kuhakikisha usalama wa raia katika Ukanda wa Gaza Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Amekiambia kituo cha utangazaji cha Marekani MSNBC jana Jumamosi kwamba, Netanyahu anafanya kosa kubwa sana kwa kutochukua hatua za kutosha za kuwalinda raia. Akasema hali hiyo inaiumiza zaidi Israel badala ya kuisaidia.

Anatoa matamshi hayo baada ya kuitolea wito Israel katika Hotuba yake ya Hali ya Kitaifa siku ya Alhamisi wa kuhakikisha inaruhusu uingizwaji zaidi wa misaada katika Ukanda wa Gaza na kuhakikisha kwamba watoa huduma za kiutu wanakuwa salama.

Biden anakabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya chama chake kinachomtaka kuwa na msimamo mkali zaidi dhidi ya Israel, ikiwa ni pamoja na kushinikiza usitishwaji wa kudumu wa mapigano.