Mioto yaendelea kusababisha uharibifu nchini Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.08.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mioto yaendelea kusababisha uharibifu nchini Ugiriki

Kikosi cha zimamoto kilikabiliana na mvuke na moshi mzito kwa siku ya saba mfululizo Jumatatu katika mji wa Pwani ya Ugiriki wa Evia ambao umekumbwa na moto mbaya zaidi wa nyikani na kuwalazimu maelfu ya watu kutoroka

Wakati mioto mingi iliyokuwa imewaka kote nchini Ugiriki kwa muda wa takriban wiki mbili ikitulia ama kupungua , ile katika eneo la misitu la Evia, kisiwa cha pili kikubwa nchini humo baada ya Crete bado inazua hofu Maafisa wa zimamoto wameliambia shirika la habari la Ugiriki la ANA kwamba serikali leo imetoa kipaumbele katika kuokoa vijiji vya Kamatriades na Galatsades kwasababu mioto hiyo ikipita katika eneo hilo, itamalizikia katika msitu mkubwa ambapo itakuwa vigumu kuuzima. Shirika la habari la AFP limeripoti kutanda kwa moshi mzito leo katika mji wa Pwani wa Pefki ambapo mamia ya watu wamehamishwa kupitia bahari.

Kikosi cha zimamoto, vikosi vya jeshi na umma, walishindwa kuendelea kupambana na moto mkali katika mji huo. "Hatuna maji" watu walipaza sauti wakati wakibeba maji yaliyokuwepo katika mikokoteni na ndoo wakati moto ukizidi kuwaka. Wafanyakazi wa kujitolea waliwabeba wazee katika pwani ambako boti zilikuwa zikiwasubiri kuwapeleka maeneo salama. Nyumba kadhaa na miti vimeteketea kwa moto na watu walijaribu kuikata miti katika baadhi ya maeneo ili kuepusha moto huo kuenea zaidi.

Griechenland l Premierminister Kyriakos Mitsotakis

Kyriakos Mitsotakis - Waziri mkuu wa Ugiriki

Kulingana na kituo cha runinga cha Ugiriki cha Skai, ndege za kikosi cha zimamoto hazikuonekana kwa saa kadhaa. Moshi mzito ulitanda katika mkoa huo huku upepo kutoka kusini ukiupuliza moto kuelekea kaskazini kuelekea kisiwa cha pili kwa ukubwa nchini Ugiriki. Wakaazi katika sehemu kubwa wamehamishwa lakini wengi wanalalamika kuwa wameachwa bila ya msaada wakati juhudi za kuzima moto kutokea angani zikianza jana Jumapili.

Waziri wa fedha Christos Staikouras amesema kuwa kiasi cha hadi euro 6,000 kitalipwa kwa familia ambazo nyumba zao ziliharibika na kiasi cha euro 4500 kwa waliojeruhiwa.

Wakati hayo yakijiri, ripoti iliyotolewa leo na jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, imehitimisha kuwa lengo la kiwango cha joto cha nyuzi 1.5 la Mkataba wa Paris linawezakukiukwa karibu mwaka wa 2030 - muongo mmoja mapema kuliko ilivyotarajiwa miaka mitatu tu iliyopita.