1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Mikopo inayohusishwa na maliasili za Afrika yakosolewa

12 Machi 2024

Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Akinwumi Adesina ametoa wito wa kukomeshwa kwa mikopo inayotolewa kwa mabadilishano ya ugavi wa utajiri wa mafuta au madini.

https://p.dw.com/p/4dRNX
Jamuhuri ya Kidemkrasia ya Kongo| Mgodi wa Mutanda Mine
Wagunia ya madini ya Cobalt yaliyohifadhiwa kwenye magunia ya kilo 500 katika Mgodi wa Mutanda wa shaba-cobalt.Picha: Emmet Livingstone/AFP/Getty Images

Adesina ameeleza kwamba mikopo hiyo imeinufaisha China kupata udhibiti wa maeneo ya uchimbaji madini barani Afrika na kuyaacha mataifa ya Afrika katika migogoro ya kifedha.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press mjini Lagos, Adesina amesema mikataba ya mikopo ya aina hii ni mibaya kwani ni vigumu kuziwekea thamani mali hizo kwa kuzingatia kuwa ni changamoto kupata bei au mkataba wa muda mrefu kwa madini au mafuta yaliyoko chini ya ardhi.

Soma pia: Adesina ni rais mpya wa Benki ya Afrika ya Maendeleo

Mkuu huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ametaja tofauti iliyopo katika mazungumzo ya mikataba, huku wakopeshaji wakiwa na mamlaka zaidi na uwezo wa kuamuru masharti ya pesa taslimu itakazoyalipa mataifa ya Afrika. Hali ambayo ukiijumuisha pamoja na ukosefu wa uwazi na uwezekano wa rushwa, inafungua njia za kutokea dhulma.

"Nina wasiwasi sana, lazima niseme, kwa Afrika kwa maana kwamba kiasi cha ufadhili wa masharti nafuu - sawa, ufadhili wa masharti nafuu wa gharama nafuu umekuwa ukipungua kwa muda. Nadhani Afrika inapaswa kukomesha mikopo inayofadhiliwa na maliasili."

Kuunganisha mapato ya baadaye kutoka kwa mauzo ya maliasili na malipo ya mkopo, mara nyingi hutajwa kama njia ya wapokeaji kupata ufadhili wa miradi ya miundombinu kutoka kwa wakopeshaji kama dhamana ili kupunguza hatari ya kutolipwa pesa zao.

Taasisi ya Adesina inayosaidia kuimarisha maendeleo katika nchi za Afrika na yenye makao yake mjini Abijan Ivory Coast imesema mipango hii inakuja na orodha ya matatizo.

Aidha Adesina amedokeza kwamba mikopo inayopatikana kupitia maliasili inaleta changamoto kwa benki za maendeleo na Shirika la Fedha la Kimataifa, ambalo linasaidia katika usimamizi endelevu wa madeni.

Uchumi wa mataifa maskini

Glencore
Kampuni ya madini ya GlencorePicha: Sigi Tischler/KEYSTONE/picture alliance

Nchi zinaweza kuhangaika kupata au kurejesha mikopo kutoka kwa taasisi hizi kwa sababu wanapaswa kutumia mapato kutoka kwa maliasili zao, ambayo kwa kawaida ni muhimu kwa uchumi wao lakini kutumia kulipa madeni yanayohusiana na mikopo ya rasilimali.

Akitolea mfano mzozo wa kifedha wa Chad, baada ya mkopo wa mafuta kutoka kwa mfanyabiashara Glencore imeliacha taifa hilo la Afrika ya kati likitumia sehemu kubwa ya mapato yake ya mafuta kulipia deni.

Soma pia: Mataifa tajiri yaahidi fedha za kuisaidia Afrika kukabiliana na tabianchi

Baada ya Chad, Angola na Jamhuri ya Kongo walifanya mazungumzo na shirika la Kimataifa la Fedha IMF kuomba msaada, lakini shirika hilo lilisisitiza majadiliano mapya katika mikataba ya mikopo yao inayofadhiliwa na maliasili.

Takriban mataifa 11 ya Afrika yamechukua mikopo yenye thamani ya mabilioni ya dola kwa dhamana ya maliasili zao tangu Miaka ya 2000, na China ndio chanzo kikuu cha ufadhili kupitia sera ya benki na makampuni yanayohusishwa na serikali.