Michael van Praag atangaza ruwaza yake ya FIFA | Michezo | DW | 04.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michael van Praag atangaza ruwaza yake ya FIFA

Mgombea wa Urais wa FIFA Michael van Praag wa Uholanzi amesema ikiwa atachaguliwa mwezi Mei atahakikisha ripoti kamili ya Michael Garcia kuhusu mchakato wa kombe la dunia 2018 na 2022 inafichuliwa

Shirikisho hilo la soka limekuwa likishinikizwa kuichapisha ripoti ya mchunguzi huyo wa maadili ili kutoa mwangaza wa kile kilichotokea wakati wa mchakato huo ambapo Urusi ilishinda kuwa mwenyeji wa mashindano ya 2018 na Qatar kunyakuwa nafasi hiyo kwa ajili ya 2022.

Van Praag ambaye ni Rais wa Shirikisho la kandanda la Uholanzi pia anataka kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki fainali za kombe la dunia kutoka 32 hadi 40, kufunguwa ofisi za uwakilishi za FIFA ili kuzisaidia maendeleo pamoja na kuvipa fedha zaidi vyama vya kandanda ,wanachama wa FIFA.

Van Praag mwenye umri wa miaka 67 alirejea tena ahadi yake ya awali kwamba atatumika kwa kipindi cha miaka minne tu pindi akichaguliwa. Akizinduwa muongozo wake wa uchaguzi mjini Zeist alisema, Hatuna budi kuhakikisha kuwa mchezo wa Kandanda unaendelea kuwa mchezo wa kila mtu.“ Tunaona flululizo wa ripoti zinazoitia dosari FIFA zikiendelea, tunashuhudia ripoti zikizimwa. Tunaona filamu za FIFA na kuihusu FIFA zikitengenezwa na kugharimu euro milioni 20 na ripoti zinazozidi kutolewa kuhusiana na vituo vya maandalizi ya kombe la dunia. huo sio ulimwengu wa kandanda anaoufahamu. Sio namna ninavyotaka kuuona mchezo huu ulionipa mengi, na ndiyo maana nagombea kuwa Rais ajaye wa FIFA . Naamini kizazi changu kina wajibu wa kuiacha taasisi hii kubwa ya kandanda katika hali bora zaidi kwa ajili ya kizazi kitakachokuja.“

Van Praag akatoa wito kuweko na uwazi katika Shirikisho hilo la kandanda la kimataifa. Uchaguzi wa rais wa Shirikisho hilo utafanyika Mei 29 mjini Zurich.

Mgombea mwengine wa Urais wa FIFA mchezaji wa zamani wa kimataifa na Ureno Luis Figo amesema yuko tayari kushiriki katika mjasdala wa televisheni pamoja na wagombea wengine watatu wa wadhifa huo.

Televisheni za Uingereza BBC na Sky, zimependekeza mjadala wa saa moja nzima akishiriki Figo, Rais wa sasa wa FIFA Sepp Blatter, Michael van Praag na Mwana Mfalme Ali Bin Hussein wa Jordan. Figo alisema kandanda linapendwa kote duniani na pana wajibu wa kuwa wazi kwa mashabiki wa mchezo huo, hivyo analiunga mkono wazo hilo. Tayari mwezi Septemba mwaka jana Rais wa FIFA Blatter alisema hana nia ya kushiriki katika mjadala wowote.

Mwandishi: Mohamed Abdulrahman/DW
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com