Miaka Mitatu Jela kwa Mubarak na 4 kwa wanawe wakiume | Matukio ya Afrika | DW | 21.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Miaka Mitatu Jela kwa Mubarak na 4 kwa wanawe wakiume

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Hosni Mubarak amekutikana na hatia ya kula rushwa na kuwaibia wananchi zaidi ya pauni 125 za Misri na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela .

Rais wa Zamani wa Misri akiwapungia mkono wafuasi wake kutoka hospitali ya kijeshi ya mjini Cairo,waliokuja kumpongeza kwa kusherehekea miaka 85 ya kuzaliwa

Rais wa Zamani wa Misri akiwapungia mkono wafuasi wake kutoka hospitali ya kijeshi ya mjini Cairo,waliokuja kumpongeza kwa kusherehekea miaka 85 ya kuzaliwa

Na wanawe pia wa kiume Gamal na Alaa wamehukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa makosa ya kutumia vibaya mali ya umma.Hukmu hizo zimetolewa miaka mitatu na nusu baada ya vuguvugu la wapenda mageuzi kukomesha miaka 30 ya utawala wa kimabavu wa Mohammed Hosni Mubarak.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 85 amehukumiwa na korti ya kwanza ya mjini Cairo kwa makosa ya kuhusika na rushwa,akituhumiwa kutumia vibaya pauni milioni 125 za Misri kutoka bajeti ya kasri la rais- kiwango cha fedha ambacho ni sawa na Euro milioni 13 na laki tano kwa ushirikiano pamoja na wanawe wawili wa kiume Gamal na Alaa.Wote,Mubarak na wanawe wametakiwa pia walipe faini ya pauni milioni 21.197 za Misri na kuamriwa kurejesha kiasi cha pauni milioni 125 ambazo korti hiyo inasema wamewaibia wananchi.

Matumaini yamemwagiwa mchanga

Ägypten Demonstration Plakat General Abdel Fattah al-Sisi

Maandamano kumuunga mkono kiongozi wa Zamani wa kijeshi,jenerali wa Zamani Abdel Fattah al-Sisi anaepigania wadhifa wa rais wa Misri

Huenda hukmu hiyo ikatuliza nyoyo kidogo za wale waliosumbuliwa na miongo mitatu ya utawala wake,lakini wadadisi wanasema matajiri wanaoendelea kumuunga mkono bado wana ushawishi mkubwa nchini humo.Na makundi yanayopigania haki za binaadam yanasema mitindo ya kimabavu ya utawala wa Mubarak inaendelea seuze tena mwanajeshi mwengine wa zamani anajiandaa kutwaa hatamu za uongozi nchini humo.

Mohammed Hosni Mubaraka anashitakiwa pia katika kesi nyengine inayohusiana na kuuliwa waandamanaji wakati wa vuguvugu la kudai mageuzi lililomng'owa madarakani mapema mwaka 2011.

Katika kesi hii ya pili rais huyo wa zamani anakabiliwa na hatari ya kuhukumiaa kifungo cha maisha jela-hukmu ambayo alikwishapewa kesi hiyo iliposikilizwa awali mwezi Juni mwaka 2012 kabla ya mahakama ya rufaa kuamua isikilizwe upya.

Mursi na wenzake wakabiliwa na hatari ya kuhukumiwa adhabu ya kifo

Mohammed Morsi Mursi Prozess Haft

Rais wa Zamani Mohammed Mursi akiwa ndani ya tundu,asikiliza kesi dhidi yake mjini Cairo

Kesi dhidi ya Mubarak zilizokuwa zikihanikiza hapo awali katika vyombo vya habari nchini Misri,zimepwaya hivi sasa na badala yake kugubikwa na zile dhidi ya aliyechukua nafasi yake,mfuasi wa kiislam Mohammed Mursi-rais pekee kuwaahi kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini Misri,na kutimuliwa madarakani na jeshi miezi 11 tu baada ya kuingia madarakani.Mohammed Mursi na takriban viongozi wote wa Udugu wa kiislam wanakabiliwa na hatari ya kuhukumiwa adhabu ya kifo katika kesi za kila aina zinazowakabili huku wafuasi wake wakiandamwa na kukandamizwa na serikali inayodhihirika kudhibitiwa na jeshi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/AP

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman