1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano tangu kufariki kwa Arafat.

11 Novemba 2009

Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi, leo wanakumbuka miaka mitano tangu kufariki kwa kiongozi aliyejulikana kama baba wa Wapalestina, Yasser Arafat.

https://p.dw.com/p/KTl8
Marehemu Yasser Arafat, akiandmana na Mahmoud Abbas.Picha: AP

Hata hivyo, Wapalestina huko Gaza hawatoanda sherehe zozote za makumbusho, baada ya chama cha Hamas kinachoongoza Gaza kufutilia mbali sherehe zozote za kumkumbuka Arafat. Miaka mitano tangu kufariki kwa Arafat, Wapalestina wamegawanyika, na ile ndoto ya Arafat ya kupatikana kwa taifa la Kipalestina bado imesalia kuwa ndoto .

Alikuwa kitambulisho cha mapambano ya uhuru wa Wapalestina, ndoto yake kuundwa kwa taifa la Palestina, na mji mkuu kuwa Jerusalem. Lakini miaka mitano tangu kufariki kwa Arafat, ambao wengi walimuita kama baba wa ukombozi wa Wapalestina- Wapalestina wamegawanyika- mamlaka aliyoongoza, chama cha Fatah kinashikilia, Ukingo wa Magharibi, Ilhali Gaza inamilikiwa na Hamas.

Flash-Galerie Jassir Arafat
Rais Bill Clinton pamoja na Yasser Arafat, pamoja na Yitzak Rabin.Picha: AP

Rais Mahmoud Abbas, mrithi wa Arafat aliyechaguliwa miezi mitatu tu, baada ya kifo cha mtangulizi wake- ameonekana kushindwa kujaza pengo aliloliacha Arafat la kuwaunganisha Wapalestina. Na unga umezidi maji, baada ya kuvunjika moyo kutokana na jinsi harakati za amani kati ya Israel na Palestina zinavyozidi kudidimia, Abbas ametangaza hatogombea urais katika uchaguzi wa Januari.

Iwapo angekuwa hai, wengi wanasema Arafat, asingeweza kustahamili, kuona Wapalestina wamegawanyika-upande mmoja wakiwa Ukingo wa Magharibi na wengine Ukanda wa Gaza. Mazungumzo ya Amani kati ya Israel na Wapalestina yamekwama miaka 14, tangu Arafat alipotia saini yale makubaliano ya amani, mjini Oslo, yaliyotoa nafasi ya uhuru wa muda kwa Wapalestina kabla ya kupatikana kwa taifa huru huru la Wapalestina.

Arafat alifariki akiwa na umri wa miaka 75, Novemba 11, mwaka wa 2004, katika hospitali mmoja mjini Paris, anakosemekana alikuwa anaugua homa ya matumbo. Kura ya maoni iliyofanywa inaonyesha aslia mia 81 ya Wapalestina, wanaoishi katika ukingo wa magharibi na hata wenzao huko Ukanda wa Gaza, wanamkumbuka sana kiongozi huyo, miaka mitano tangu aondoke.

'' Arafat alikuwa kiongozi shujaa, kitambulisho cha watu wa Palestina. Hatuwezi tukamsahau, anasema Hasan Rushdi, ambaye alifunga safari kutoa heshima zake katika kaburi la Arafat huko Ramallah.

Palästinenser Israel Westjordanland Jassir Arafat Plakat
Wafuasi wa Arafat, huko Ramallah.Picha: AP

'' Niko hapa kumuambia ahsante baba wa Wapalestina, kwa kuzipa sauti harakati za ukombozi wa Wapalestina. Nataka kumuambia tumukosa sana uongozi wake, aliongeza Rushdi.

Huko Ukingo wa Magharibi, wameandaa mikutano mikubwa kumkumbuka, Arafat waliyempa jina la Qaida kwa lugha ya kiarabu, lenye maana ya Kiongozi. Kuna tofauti kubwa jinsi Wapalestina walivyomtambua Arafat na mrithi wake Abbas. Abbas wanamtambua tu kama rais, mkuu wa utawala wa Palestina. Huko Gaza, Wapalestina watamkumbuka Arafat, pengine majumbunai mwao tu, kwani chama cha Hamas kimefutilia mbali makumbusho yeyote ya kiongozi aliyechukuliwa kama nyota, na mkombozi wa ile ndoto ya taifa huru la Palestina.

Mwandishi: Munira Muhammad/ DPAE

Mhariri- Abdul-Rahman.