Mgomo wa wafanyakazi wavuruga safari za ndege Nairobi | Matukio ya Afrika | DW | 06.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mgomo wa wafanyakazi wavuruga safari za ndege Nairobi

Shughuli za usafiri zimevurugika katika uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya kufuatia mgomo wa wafanyakazi wanaopinga usimamizi wa uwanja huo kutwaliwa na Shirika la Usafiri wa ndege ya Kenya.

Wasafiri wengi katika uwanja huo wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi katika eneo la Afrika chini ya jangwa la Sahara wa Jomo Kenyatta, walikumbana na zogo la mgomo wa wafanyakazi wa uwanja huo, bila kutarajia.

Mgomo huo ulioanza usiku wa manane, umeathiri shughuli katika viwanja vya ndege vya miji ya Mombasa, Kisumu na Eldoret kutokana na ndege kushindwa kusafiri kwa wakati.

Kenia Streik der Kenya Aviation Workers Union (DW/S. Wasilwa)

Wafanyakazi wa shirika la ndege la Kenya wakosa la kufanya kufuatia mgomo wa wafanyakazi katika Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta

Wafanyakazi wanaopinga usimamizi wa uwanja huo kutwaliwa na Shirika la Usafiri wa ndege ya Kenya wanasema hii wanadai huenda ikachangia wengi wao kukosa ajira.

Moses Ndiema ni katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa mashirika ya usafiri wa angani nchini Kenya, alisema haya kabla ya kukamatwa na polisi.

"Wafanyakazi wa uwanja huu ndio wamefanya hali kuwa hivi ilivyo, sisi ni wengi, na wasipotupatia tutajichukulia, tumeweka misururu ya mikutano tukiwaambia waje tongee, na kama leo wanataka tuongee waje hapa,” alisema Moses Ndiema katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa mashirika ya usafiri wa angani nchini Kenya.

Shirika la Ndege nchini Kenya, lina mipango ya kuingia ubia na Mamlaka ya Viwanja vya ndege ili kuvisimamia. Jumatatu waziri wa Uchukuzi James Macharia alikanusha madai kuwa Shirika la ndege la Kenya, linaendesha ndege zinazosimamiwa na baadhi ya watu wanaopanga kuchukua usukani wa viwanja vya ndege nchini.

Awali Shirika la ndege la Kenya, liliwaonya wasafiri juu ya matatizo ya usafiri

Wafanyikazi wa Viwanja vya ndege wanataka usimamizi wa Shirika la ndege la Kenya pamoja na Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege ubadilishwe. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Shirika la ndege la Kenya, limeonya wasafiri watarajie matatizo ya usafiri siku ya Jumatano. Sebastian Mokosz anasema kuwa, hali inashughulikiwa.

Kenia Streik der Kenya Aviation Workers Union (DW/S. Wasilwa)

Abiria waliokwama katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi

"Hali ilivyo sasa ni kwamba, kuna wasafiri ambao wanaingia, kwa hivyo lazima tusubiri wasafiri wote, kabla ya kuondoka, na hatutaondoka kabla ya wasafiri wote kufika, lakini natarajia kuwa mwisho wa siku mambo yatakuwa mazuri," alisema Sebastian Mikosz.

Muungano wa wafanyikazi hao, umehoji ni vipi Shirika la Ndege la Kenya litachukua usimamizi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege ilhali limekuwa likipata hasara ya mabilioni ya fedha kila mara. Muungano huo unasema kuwa hatua hiyo itachangia hasara ya mabilioni ya fedha huku wafanyakazi wengi wakipoteza ajira.

Kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita, Katibu Mkuu mtendaji wa Shirika la Ndege la Kenya, Sebastian Mikosz, mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo Michael Joseph na wakurugenzi kadhaa wamelipwa dola milioni 13, hali inayotiliwa shaka na Muungano wa wafanyikazi. Wanataka wasimamizi hao kutimuliwa kwa ubadhirifu wa fedha. Serikali inamilikia asilimia 46.5 ya hisa katika Shirika la ndege la Kenya huku benki 11 zikimilia asilimia 35.6

Mwandishi: Shisia Wasilwa

Mhariri: Iddi Ssessanga