Mchakato wa kuunda serikali waanza Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 24.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mchakato wa kuunda serikali waanza Kenya

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, yuko katika harakati ya kuunda serikali yake kwa kuanza kutaja majina ya mawaziri wanne kati ya mawaziri 18 watakaokuwepo katika baraza lake la mawaziri.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Baraza la mawaziri nchini Kenya awali lilijumuisha mawaziri 44. Hapo jana Rais huyo mpya aliyechaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Machi 4 nchini humo, alimteau mwanadiplomasia Amina Mohammed kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje.

Amina ambaye ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa katika nafasi hiyo tangu Kenya ijinyakulie Uhuru wake mnamo mwaka wa 1963, alianza taaluma yake katika wizara hiyo kisha akajiendeleza kupitia wizara ya sheria.

Kabla ya kujiunga na Umoja wa Mataifa, Amina alikuwa akiwania nafasi ya Pascal Lamy ya kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la biashara duniani, WTO, kabla ya kuchujwa katika nafasi hiyo mapema mwezi huu.

Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto

Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto

Waziri mwengine aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa katika baraza lake la mawaziri ni Henry K. Rotich, kuongoza wizara ya Fedha.

Rotich ambaye ni msomi na mchumi alifanya kazi kwa muda mrefu katika wizara ya fedha nchini Kenya na hata katika Benki kuu ya nchi hiyo.

Mawaziri wengine wawili walioteuliwa hapo jana ni pamoja na waziri wa Mawasiliano Daktari Fred Okeng'o Matiangi na waziri wa Afya Bwana James Wanaina Macharia.

Rais Uhuru Kenyatta amesema mawaziri wengine 14 watatajwa baadaye. Rais Uhuru hakutaja tarehe kamili ya kutangaza majina hayo.

Kamati ya bunge kuwachuja mawaziri wateule

Hata hivyo kabla wanne hao walioteuliwa kuthibitishwa kuwa mawaziri kamili ni lazima wapitie mchujo katika kamati ya bunge inayoongozwa na Spika wa Bunge, Justin Muturi.

Bunge la zamani la Kenya

Bunge la zamani la Kenya

Majina hayo ya mawaziri wateule yalitangazwa saa chache baada ya bunge kuunda kamati ya wabunge 28 ya kuwachuja mawaziri watakaoteuliwa na rais Uhuru Kenyatta. Kulingana na katiba ya Kenya ni lazima majina ya maafisa wakuu wa serikali, wakiwemo mawaziri, mabalozi na wakuu wa tume za kikatiba, wapitishwe na kamati ya bunge.

Huku hayo yakiarifiwa wataalamu nchini Kenya wanasema huenda mawaziri walioteuliwa hapo jana wakapitishwa bila pingamizi lolote kutokana na kamati hiyo ya bunge iliyoteuliwa kufanya mchunjo huo kujumuisha wabunge 16 wa muungano wa Jubilee wake Uhuru Kenyatta na wabunge 10 kutoka kwa muungano wa Cord. Kamati hiyo pia ina mwanachama mmoja ambaye haegemei upande wowote.

Rais Kenyatta aahidi kuinua uchumi wa nchi

Rais Uhuru Kenyatta awali aliahidi kuimarisha marudufu uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kuwaondoa katika umaskini Wakenya milioni 10 kati ya milioni 40 idadi ya raia wa nchi hiyo ifikapo mwaka wa 2017.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Uchaguzi wa amani uliompa ushindi Uhuru Kenyatta pamoja na makamu wake wa rais, William Ruto, uliofanyika Machi nne mwaka huu nchini Kenya, umebadilisha soko la biashara na kufuta japo kwa pole pole kumbukumbu ya ghasia zilizotokea katika uchaguzi wa mwaka 2007 na 2008 ambapo watu zaidi ya 1,200 waliuwawa.

Katika Ghasia hizo pia watu wengi waliachwa bila makaazi nchini humo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza