Mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi yaanza Bonn | Masuala ya Jamii | DW | 01.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi yaanza Bonn

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius ameufungua rasmi hapa Bonn, Ujerumani, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi unaolenga kufikia mwafaka kudhibiti gesi chafu

Mkataba huo kisha utakamilishwa mjini Paris baadaye mwaka huu. Kufikia lengo la nyuzi joto mbili limekuwa suala kuu kwa wajumbe wa mazungumzo ya tabia nchi na wanasayansi, ambao wanasema ndicho kikomo ambacho kupindukia kwake kutaufanya ulimwengu ukabiliwe na majanga yanayoendelea kutokea ya mafuriko, ukame, na vimbunga.

Lakini ikiwa imesalia miezi sita kabla ya viongozi wa ulimwengu kukutana mjini Paris, matarajio yanadidimia ya kupatikana muafaka ambao utaweka kiwango cha wastani cha joto chini ya kikomo hicho. Uzalishaji wa gesi chafu umefikia viwango vya juu kabisa katika miaka ya karibuni.

Klimakonferenz UNFCCC Bonn 2014

Jumba la Mikutano ya Kimataifa mjini Bonn

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius ameufungua mkutano wa Bonn wa siku kumi ambao utaendelea kutathmini mafanikio ya kuzishughulikia mbinu mwafaka za kuimarisha atua za mabadiliko ya tabia nchi kabla ya 2020, mwaka ambao mkataba mpya utaanza kutekelezwa.

Rasimu ya sasa ina kurasa 80 za mitazamo ya kitaifa, mingine ambayo inaingiliana na kutoa misimamo inayotofautiana. Lengo la mkutano wa Bonn ni kuwasilisha mkataba ambao utaokoa hali ya hewa ya ulimwengu dhidi ya uharibifu unaotokana na joto kali linalosababishwa na gesi chafu. Mkataba huo utazitaka nchi wanachama kuweka sheria za kudhibiti uzalishaji wa gesi chafu na kuzisaidia nchi maskini ambazo zinakabiliwa na kitisho cha ukame, mafuriko na kupungua kwa viwango vya maji barahini.

Baadhi ya nchi zinataka kuweka malengo ya hatua kwa hatua na mataifa 38 pekee - ikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya, Urusi na Canada – yameahidi kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Mkataba unaotafutwa utazifungamanisha kisheria zaidi ya nchi 190 kabla ya kuanza kutekelezwa mwaka wa 2020.

Mkutano wa kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda ulimwenguni – G7, utakaoandaliwa katika jimbo la Bavaria hapa Ujerumani mnamo Juni 7-8, huenda pia ukayajadili mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa.

Christiana Figueres,mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi anasema serikali zinahitaji kubadilisha mitazamo yao na kutegemea uchumi unaotokana na kiwango cha chini cha kaboni, kwa kuzingatia nishati safi kama vile upepo au nguvu za jua, ambazo zinaweza kuimarisha ukuwaji uchumi, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kubuni nafasi za kazi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com