Matumaini ya muungano wa Afrika nzima miaka 50 ijayo | Matukio ya Afrika | DW | 24.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Matumaini ya muungano wa Afrika nzima miaka 50 ijayo

Terehe 25 Mei 1963, Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia aliwaambia viongozi 31 wa Kiafrika katika uzinduzi rasmi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kwamba "Afrika ipo nusu ya safari katikati ya jana na kesho."

Emperor of Ethiopia Haile Selassie is shown during an interview in the Grand Palace, Addis Ababa, Ethiopia in 1974. (AP Photo)

Haile Selassie

Kuanzishwa kwa OAU miaka 50 iliyopita kilikuwa kitendo cha kihistoria na mwanzo wa bara la Afrika kupambana na ukoloni kwa sauti moja. Mkutano huo ndio ulioiasisi OAU na kupewa jina la "chanzo cha ndoto" ya bara zima la Afrika.

Akiwahutubia viongozi waliohudhuria katika mkutano huo, Mfalme Haile Selassie alisema "kipindi cha kutawaliwa, kunyanyaswa, kudhulumiwa na kuwafanywa watumwa kwa watu wa bara la Afrika kimepita. Leo Afrika imeibuka kutoka gizani na inaanza vita vya kupambanua kati ya heri na shari."

Kauli hiyo ya Mfalme Haile Selassie ilipata mashiko siku hadi siku tangu kuasisiwa kwa Umoja huo. Angola na Msumbiji, chini ya viongozi wa kupigania ukombozi, zilipambana na kuung'oa utawala wa kikoloni wa Mreno.

Zimbabwe na Namibia nazo zikapambana na kupata uhuru, na miaka isiyopungua 30 tangu mkutano wa kuasisi OAU, Afrika ya Kusini nayo iliiangusha serikali ya wachache iliyokuwa ikifuata misingi ubaguzi wa rangi na serikali ya mpya ya walio wengi ikaingia madarakani.

Ndoto ya Gaddafi, ndoto ya Afrika

Aliyekuwa kiongozi wa Libya na mwanzilishi wa wazo la sasa la Umoja wa Afrika, Muammar Gaddafi.

Aliyekuwa kiongozi wa Libya na mwanzilishi wa wazo la sasa la Umoja wa Afrika, Muammar Gaddafi.

Umoja wa Nchi Huru za Afrika ulibadilishwa jina na kuwa Umoja wa Afrika mwaka 2002, katika mkutano mkuu wa viongozi hao uliyofanyika Durban, Afrika ya Kusini.

Msingi wa mageuzi hayo ni wazo la kiongozi wa wakati huo wa Libya, Muamar Gaddafi, kwamba OAU kilikuwa chombo kilichopoteza nguvu kwani kilishindwa kutatua migogoro na vita katika nchi wanachama, akipigia mfano wa mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.

Matokeo ya wazo hilo la Gaddafi hayakuwa tu kubadilishwa jina na Umoja huo, bali pia kubadilika muelekeo wa kimahusiano kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

Sasa viongozi wa sasa wa Umoja huo wamekuwa na ushirikiano zaidi katika kuzijenga nchi zao kijamii, kisiasa na kiuchumi, ili kufika lengo la kuwa sarafu moja, jeshi moja la kulinda amani, bunge moja na vile vile kuwa na mahakama ya haki za binadamu.

Changamoto mpya

Mkuu wa Kamisheni ya Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.

Mkuu wa Kamisheni ya Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.

Nusu karne sasa tangu ukoloni kuanza kujiondoa barani Afrika chini ya shinikizo la Umoja huo, bara hilo sasa linakumbana na changamoto nyingi zaidi kuliko hapo awali, ukiwemo umasikini na njaa, athari za mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa kazi na migogoro na vita ya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea katika za nchini Mali, Sudan na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Japokuwa kuna changamoto hizo, wanadiplomasia kutoka Afrika wanasema kuwa mpango na utaratibu wa kuiunganisha Afrika yenye amani haujashindikana, bali ni mchakato unaoendelea.

Akizungumzia kuhusu changamoto hizo, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosana Dlamini Zuma, amesema kama viongozi waasisi wa Umoja huo walivyokutana mwaka 1963 na kuamua kupambana ili kupata uhuru wa kisiasa, mwaka 2013 Afrika ipo katika mchakato wa kuleta amani na utulivu kwa watu wake.

Ili kutimiza malengo hayo, Umoja wa Afrika umeanzisha kampeni inayoitwa 2063 yenye lengo la kuwataka na kuwaomba Waafrika kuchangia mawazo yao kuelekea Afrika moja na imara ndani ya miaka 50 ijayo. Hiyo itakuwa ni moja ya ajenda katika kikao cha viongozi wa juu wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, Januari 2014.

"Kunatakiwa kuwepo na Afrika isiyohitaji misaada na isiyo na njaa na Afrika yenye kujiamini na kujidai ifikapo mwaka 2063." Amesema Kamishna wa Masuala ya Kilimo wa Umoja wa Afrika, Rhoda Tumusiime.

Mwandishi: Rukundo Laurance /DPE
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza