Matumaini ya kuwapata manusura wa maporomoko Papua yafifia
28 Mei 2024Umoja wa Mataifa unasema kuna uwezekano mdogo sana wa kuwapata manusura wa maporomoko ya udongo nchini Papua New Guinea, ukiwaonya wakaazi walio kwenye maeneo yaliyo hatarini kuondoka. Zaidi ya watu 2000 wanahofiwa kuzikwa kwenye maporomoko hayo ya udongo.
Soma zaidi. Watu wahamishwa kutoka maeneo hatari Papua New Guinea
Kwa siku kadhaa, wakaazi wa Papua New Guinea wamekuwa wakipambana kwa kila hali katika eneo lililokumbwa na maporomoko ya ardhi kuwatafuta wapendwa wao ambao wamefukiwa na maporomoko hayo.
Mwakilishi wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF katika visiwa hivyo, Niels Kraaier, amesema hadi sasa matumaini ya kuwapata manusura hao yanazidi kufifia, juhudi kamili za uokoaji na usaidizi zimetatizwa pakubwa na umbali wa eneo hilo, mvua kubwa na ghasia za kikabila zilizo karibu na eneo la maporomoko ya udongo.
Mapema leo, msimamizi wa jimbo la Enga, Sandis Tsaka, akizungumza na shirika la habari la AFP alionya kuwa bado maporomoko yanaendelea katika eneo la Mlima Mungalo na kwamba kwa sasa wanafanya jitihada za kuwahamisha watu 7,900.
Soma zaidi. Papua New Guinea yaripoti watu zaidi ya 2000 wamefukiwa na matope
Albanese: Australia imejitolea kuisaidia Papua New Guinea
Akizungumzia mkasa huo Waziri Mkuu wa Australia Antony Albanese amesema nchi yake inajitolea kukisaidia kisiwa hicho jirani.
"Serikali inatoa msaada wa kibinadamu ili kuunga mkono jitihada za Papua New Guinea ninamshukuru kiongozi wa upinzani (Peter Dutton) kwa kuonyesha kwamba bila shaka misaada hiyo itakuwa ya pande mbili. Mchana wa leo, tunatuma wataalam wa kiufundi kutoa msaada wa usimamizi wa matukio kusaidia kufanya tathmini ya hatari na kusaidia kuelekeza juhudi za uokoaji amesema Antony Albanese.
Mbali na kauli hiyo, Australia imetangaza misaada yenye thamani ya mamilioni ya dola, ikijumuisha vifaa vya dharura kama vile malazi, vifaa vya usafi na msaada kwa wanawake na watoto.
Soma zaidi. Waokoaji wapambana kuwatafuta manusura Papua New Guinea
Mapema leo mamlaka ya Papua New Guinea imefanya mkutano kwa njia ya mtandao na Umoja wa Mataifa na washirika wa kimataifa katika juhudi za kuongeza misaada zaidi.
Mpaka sasa idadi ya vifo inayokadiriwa imeongezeka tangu maafa hayo yalipotokea, huku maafisa wakiendelea kufanya tathmini ya ukubwa wa mkasa huo.