Matamshi ya Rais Magufuli yazusha hisia mseto Uganda | Matukio ya Afrika | DW | 09.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Matamshi ya Rais Magufuli yazusha hisia mseto Uganda

Rais Magufuli alinukuliwa akisema, angekuwa na uwezo, angewachukulia hatua watendaji wanaotatiza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Tanzania na Uganda.

Matamshi ya rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kuhusu chanzo cha kusitishwa kwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kati ya nchi yake na Uganda yamepokelewa kwa maoni mbalimbali na raia wa Uganda.

Katika kongamano la kibiashara kati nchi hizo mbili lililofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli alinukuliwa akisema, angekuwa na uwezo, angewachukulia hatua watendaji wanaotatiza mradi huo.

Tamko hilo limefasiriwa na baadhi ya raia wa Uganda kuwa angalau Magufuli akipewa fursa ya kuitawala Uganda kwa wiki moja, angeondoa urasimu unaotatiza mradi huo wa ujenzi wa bomba la mafuta kutokana na mashaka ya kodi.

Mradi huo wa ujenzi wa bomba la mafuta wa thamani ya dola bilioni 3.6 za kimarekani kutoka Hoima magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania umesitishwa baada ya kampuni ya Total E and P ya Ufaransa kuamua kutoendelea nao kufuatia mashaka ya kuanzishwa kwa uchimbaji mafuta. Mashaka hayo yaliibuka pale kampuni ya Tullow ilipotupilia mbali mpango wa kuyauzia makampuni ya uchimbaji mafuta ikiwemo CNOOC ya China asili mia 21 ya biashara yake.

Hii ilikuwa baada ya mamlaka ya mapato ya Uganda URA pamoja na mashirika mengine ya serikali kutaka makampuni hayo kulipa kodi ya kiasi cha dola milioni 185 ili kuweza kuendesha muamala huo. Kulingana na rais Magufuli, mashirika ya serikali ya Uganda yangefaa kuzingatia manufaa ya mradi huo badala ya hiyo kodi.

Ni kwa ajili hii ndipo wazo likaibuka miongoni mwa raia wa Uganda kwamba Rais Magufuli angekuwa na uwezo wa kutawala Uganda angalau kwa wiki moja hakikisha kuwa mradi huo hautatizwi na urasimu. Baadhi wametoa maoni kwa kumuunga mkono Magufuli wakisema kuwa, bomba hilo la mafuta lingeiunua uchumi wa mataifa hayo mawili na hivyo basi kupe.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Pia wamesema kuwa mradi huo ungetoa ajira kwa vijana kama wafanyakazi katika sekta ya mafuta.

Waganda wamemtaka rais Museveni afuate ushauri wa Magufuli kwa kuwafukuza baadhi ya wafanyakazi katika mamlaka ya mapato, ambao wamezorotesha ujenzi wa bomba la mafuta kati ya nchi hizo mbili kwani wameathiri ukuaji wa uchumi wa Afrika mashariki

Suala la urasimu katika mashirika na wizara za serikali mara nyingi limetajwa na wananchi kuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi za mataifa kadhaa Afrika. Msingi wa mjadala wa aina hii ni kwamba panapo na fursa kama hiyo ya mradi ambao manufaa yake ni makubwa kwa wananchi, sera na sheria fulani zisizingatiwe.

Kwa mfano chini ya mradi huo mkubwa zaidi kati ya Uganda na Tanzania, raia wengi wangenufaika kutokana na fursa za kazi za ujenzi hata kabla ya shughuli kamili ya uchimbaji na usafirishaji mafuta kupitia bomba hilo la urefu wa kilomita 1,445.

Mamlaka ya mapato Uganda iliyataka makampuni hayo kulipa kodi kutokana na mauzo ya dola milioni 900 za kimarekani kati yao.

Kwa mtazamo wa rais Magufuli dhana ya kulipwa kwa kodi hiyo haizingatii faida kubwa ya baadaye na tija endelevu ya biashara ya mafuta.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.