Urusi yadungua droni 251 zilizoathiri huduma ya umeme
6 Oktoba 2025
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, droni 251 za Ukraine zilidunguliwa zilipoingia anga yake na Rasi ya Crimea usiku wa kuamkia Jumatatu. Mabaki ya droni zilizodunguliwa yalisababisha moto kwenye kiwanda cha kuchakata mafuta cha Tuapse lakini moto huo ulizimwa baada ya muda usiokuwa mrefu. Kiwanda hicho huzisambazia mafuta China, Malaysia, Singapore na Uturuki.
Kulingana na Gavana wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov kupitia jukwaa la Telegram Jumapili jioni, mitambo ya nishati iliharibiwa kwenye shambulio hilo na hadi Jumatatu asubuhi, wakaazi wa maeneo 24 hawakua na umeme licha ya kushughulikiwa usiku kucha.
Ukraine yasema Urusi iliiwashambulia
Gavana wa eneo la Kharkhiv lililoko mashariki, Oleh Syniehubov aliandika kwenye Telegram kuwa watu 4 walijeruhiwa na baadhi yao wanakabiliana na kiwewe.
Duru za kijeshi za Ukraine zinaeleza kuwa Urusi iliwavamia kwa droni 116 za mapambano na 86 kati ya hizo zilidenguliwa.Kwa jumla yalifanyika mashambulio 30 kwenye maeneo 7 zinaeleza duru rasmi.
Ifahamike kuwa Ukraine imekuwa ikijilinda na mashambulizi ya Urusi kwa muda wa miaka mitatu u nusu sasa na kulazimika kulipiza kisasi kwa kuvamia viwanda vyao vya nishati. Vyombo vya habari vya Ukraine viliripoti kuwa moto mkubwa uliwaka pale bohari la mafuta liliposhambuliwa kwenye eneo la Feodosia la pwani ya Crimea.
Medvedev: Urusi haihusiki kuvuruga usafiri wa anga
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev ambaye ni naibu mwenyekiti wa baraza la Usalama alipuuzilia mbali madai dhidi ya nchi yake ya kuvuruga usafiri wa anga barani Ulaya.
Urusi imeghadhabishwa na kauli za mataifa ya Ulaya za kupendekeza matumizi ya mali yake kufadhili ununuzi wa silaha mahsusi kwa Ukraine kudengua ndege zao kadhalika kuunda ukuta wa ulinzi dhidi ya mashambulizi ya droni.Urusi inashikilia haina nia yoyote ya kuvamia nchi yoyote mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO.