1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mashambulizi nchini Urusi yaharibu dhana ya 'jeshi la Putin'

5 Juni 2023

Mashambulizi ya hivi karibuni ya kutumia droni na makombora dhidi ya mji wa mpakani wa Urusi, yalizusha hofu na kusababisha wakaazi kuyakimbia makaazi yao.

https://p.dw.com/p/4SDBj
Russland Evakuierung von Kindern aus der Region Belgorod
Picha: Mikhail Tokmakov/TASS/dpa/picture alliance

Utawala wa Urusi umepuuza mashambulizi hayo, lakini wataalam wanafikiri yanafichua udhaifu wa Putin.

Shebekino, mji wenye wakaazi 40,000, upo kilomita tano ndani ya Urusi kutoka kwenye mpaka wa kusini magharibi mwa nchi hiyo na Ukraine. Wakaazi wake wamesema katika miezi michache iliyopita, mji huo umeshambuliwa mara kwa mara. Lakini shambulizi la hivi karibuni siku ya Alhamisi halikutarajiwa na ukubwa wa mashambulizi hayo yaliuharibu mji huo na kusababisha nusu ya wakaazi wake kukimbia.

Picha na video zilizosambazwa mitandaoni zilionesha mitaa iliyojaa moshi, majengo yaliyoharibiwa na barabara zilizofunikwa kwa mabaki ya makombora.

Kulingana na maafisa, wanawake wawili waliuawa na watu wasiopungua 12 walijeruhiwa.

Wanamgambo wanaounga mkono Ukraine wanaojitambulisha kama Kikosi kinachopigania uhuru Urusi na Jeshi la Kujitolea la Urusi, walidai kuingia kwenye mji wa Shebekino siku ya Alhamisi, wakisema wangeikomboa Urusi Yote, kutoka Belgorod hadi Vladivbostok.

Mashambulizi ndani ya Urusi yanazidi kuwa ya kawaida

Serikali ya Ukraine ilikana kuhusiana kwa vyovyote vile na wanamgambo hao, japo afisa mmoja wa jeshi la Ukraine amekiri "kushirikiana” na makundi hayo.

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine

Mapema mwezi Mei, makundi haya ya "kujitolea” na yanayodaiwa kuundwa na wapiganaji wa Urusi wanaopigana kwa kuunga mkono Ukraine, yalifanya uvamizi katika eneo la mapambano la Belgorod.

Wachambuzi wengi walitizama mashambulizi hayo kuwa fedheha kwa serikali ya Urusi, na yaliibua wasiwasi kwamba maeneo ya mstari wa mbele nchini Urusi yanaweza kushambuliwa.

Kufuatia ongezeko la uvamizi ndani ya Urusi katika wiki za hivi karibuni, unaofanywa na wanamgambo, baadhi ya wakaazi wa Belgorod wamemtaka gavana wao kutangaza hali ya hatari katika eneo hilo. Hatua hiyo itawawezesha kupata fidia kutoka serikalini.

Wakaazi wasema hawajui nani atawalinda

Waliliambia shirika hili la habari la DW kwamba wanahisi serikali imewaacha nyuma. Mkaazi aliyejitambulisha kwa jina Svetlana ameuliza swali "je serikali inatuhitaji? Wanawatizama watu walioko maeneo ya mipakani kama wanaoweza kutupwa”.

Kwenye mazungumzo ya DW, baadhi ya wakaazi walikosoa vikali vita vya Ukraine. Alina ambaye hakutaka kutaja majina yake yote amesema wanapaswa kuviondoa vikosi vyao katika nchi nyingine, "turudishe rasi ya Crimea na maeneo mengine ya Ukraine ambayo yamenyakuliwa, na kwamba maafisa wanapaswa kwanza kuwatumikia raia wao.

Ukraine yaendelea kuyakomboa maeneo yake

Lakini hawawezi kuyasema hayo waziwazi kwa sababu walieleza kuwa wao ni miongoni mwa wachache huko Shebekino.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, hajaelezea wasiwasi wake hadharani kuhusu mashambulizi hayo ya mpakani.

Msemaji wa serikali yake Dmitry Peskov alipoulizwa kuhusu mashambulizi hayo alionekana kuyapuuza alipojibu kwamba, hayawezi kuathiri operesheni yao maalum ya kijeshi nchini Ukraine.

Tatiana Stanovaya, mchambuzi wa siasa ambaye pia ni mtaalamu katika taasisi inayojihusisha na masuala ya amani ya kimataifa Carnegie Endowment, aliandika kwamba mkakati wa Putin ni kunyamaza kimya pale inapowezekana na asijikite kwenye mashambulizi, ili kufanya kushindwa kwake kuonekana kama mafanikio.

Stanovaya anahisi mikakati ya Putin imeanza kufeli. Watu wanataka kuona uongozi wenye nguvu, lakini kwa sasa uongozi wake unaonekana kuhitaji misaada na kuchanganyikiwa zaidi.

Abbas Gallyamov ambaye pia ni mchambuzi wa siasa na aliyekuwa mwandishi wa hotuba za Putin zamani pia anadhani mashambulizi ya hivi karibuni ndani ya Urusi yanaweza kuwa na athari katika mitizamo ya umma kuhusu uongozi wa Urusi na vita nchini Ukraine.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, amesema "mashambulizi huko Belgorod yanaharibu kabisa dhana ya kile kinachotajwa kuwa jeshi lisiloweza kushindwa la Putin. Hawajui tu jinsi ya kusonga mbele, lakini pia ni mbaya katika ulinzi".