1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya yatokea Nagorno-Karabakh

8 Oktoba 2020

Mapigano kati ya vikosi vya Armenia na Arzerbaijan zinazowania udhibiti wa jimbo la Nagorno-Karabakh yameendelea hadi leo, huku kukishuhudiwa mashambulizi mapya ya mabomu katika mji mkuu wa jimbo hilo

https://p.dw.com/p/3jd6t
Berg-Karabach Konflikt
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Kulingana na waandishi wa habari wa shirika la AFP miripuko na ving'ora imeendelea kusikika katika mji mkuu Stepanakert. Raia kadhaa wamethibitishwa kuuwawa na upande wa Armenia umekiri kwamba zaidi ya wanajeshi wake 300 wameuwawa.

Azerbaijan haijatangaza kifo chochote miongoni mwa majeshi yake. Maafisa mjini Baku walisema jana kuwa nyumba 427 ambazo ni makaazi ya karibu watu 1,200 zimeharibiwa. Soma pia: Uturuki yaitaka dunia kuiunga mkono Azerbaijan

Kwa upande wake, jumuiya ya kimataifa imeendelea kupaza sauti yake kutaka mapigano yasitishwe mara moja na hapo jana Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema kuibuka tena kwa mapigano eneo hilo ni janga.

Ila kwa sasa hakuna dalili za mapigano hayo kupunguwa na hatua ya Uturuki kuiunga mkono Azerbaijan imezua hofu katika nchi za Magharibi kwamba huenda mapigano hayo yakageuka na kuwa vita kamili kati ya Uturuki na Urusi ambayo ina makubaliano ya kijeshi na Armenia.

Berg-Karabach Konflikt
Ganda la kombora kutokana na mashambulizi ya karibuniPicha: Reuters

Maafisa wa ulinzi kutoka pande zote wanasema mapigano bado yanaendelea huku kila upande ukisema umesababisha hasara kubwa kutokana na mashambulizi yake. Pande hizo aidha zinalaumiana kwa mashambulizi yaliyofanyika katika maeneo ya makaazi ya raia.

Mbali na mashambulizi hayo mapya, Azerbaijan inasema mabomu ya Armenia yamesababisha vifo na watu kadhaa kujeruhiwa katika vijiji walivyovishambulia. Soma pia: Mkuu wa NATO ataka mapigano yasitishwe Nagorno-Karabakh

Waziri wa nchi za nje wa Azerbaijan Jeyhun Bayrov atakutakana na wanadiplomasia kutoka Ufaransa, Marekani na Urusi leo ambapo pamoja wanaunda lile "kundi la Minsk” ambalo limekuwa likitafuta mwafaka katika huo mzozo wa Karabakh tangu miaka za tisini.
Waziri wa mambo ya nje wa Armenia hatohudhuria mkutano huo baada ya nchi yake kuondoa uwezekano wa mazungumzo kati ya wanadiplomasia wakuu wan chi hizo mbili kipindi mapigano yakiwa bado yanaendelea.

Mapigano hayo ya zamani yaliyoanza baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Sovieti yalikuwa yametulia kwa muda ila yakaibuka tena Septemba 27 huku Azerbaijan ikisisitiza kuwa eneo la Nagorno Karabakh lirejee katika udhibiti wake. Soma pia: Mapigano ya Armenia-Azerbaijan yapamba moto

Mkoa huo ulijitenga kutoka Azerbaijan katika miaka ya tisini katika vita vilivyosababisha mauaji ya watu 30,000. Watu waliokuwa wanataka kujitenga kutoka Armenia walitangaza kupata uhuru wao wakati huo ila hakuna nchi inayotambua utawala wake na Nagorno-Karabakh bado inatambulika na viongozi wa dunia kama sehemu ya Azerbaijan.

afp, dpa, ap, reuters