1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 280 wauwawa Nagorno Karabakh

Saumu Mwasimba
7 Oktoba 2020

Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan ameilaumu Uturuki kwamba inaendeleza sera za mauaji ya jamii ya Warmenia ili kuweka himaya yake katika ukanda huo

https://p.dw.com/p/3jYMA

Wizara ya ulinzi ya jimbo la Nagorno Karabakh imesema wanajeshi wake 280 wameuwawa hadi sasa katika mapigano na Azerbaijan. Leo peke yake wanajeshi 40 wa Karabakh ni miongoni mwa waliouwawa.Jumuiya ya kimataifa imeendelea kutowa mwito wa kusitishwa kwa mapigano hayo.

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametowa mwito leo Jumatano akitaka mapigano hayo yasitishwe katika jimbo la Nagorno Karabakh akisema ni mapigano mabaya zaidi yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu ambayo hayajawahi kuonekana kwa zaidi ya miaka 25.

BdTD Berg-Karabach Konflikt
Picha: Pablo Gonzalez/Agencia EFE/Imago Images

Putin ameyaita mapigano kati jamii ya  Warmenia na wanajeshi wa Azerbaijan kuwa ni masikitiko makubwa.Katika mahojiano yaliyooneshwa kwenye televisheni rais huyo wa Urusi amesema anawasiliana muda wote  na waziri mkuu wa Armenia Nikol Peshinyan kuhusu mgogoro huo.Waziri mkuu huyo wa Armenia anasema vitendo vya Uturuki na Azerbaijan vimeongeza mashambulizi ya kigaidi katika jimbo Nagorno Karabakh ambayo yametengeneza  sehemu ya muendelezo wa mauaji ya halaiki ya watu wa Armenia.

''Tunachokabiliana nacho ni mashambulizi ya kigaidi ya Kimataifa ya Azerbaijan na Uturuki  dhidi ya Nagorno Karabakh. Na nafikiri hili sio tena suala la eneo hili peke yake. Tazama hata ufaransa imekiri kwamba kuna magaidi wanane mamluki walioletwa kutoka Syria,jamhuri ya kiislamu ya Iran na Urusi imethibitisha hilo''

Msimamo wa Uturuki

Uturuki kupitia waziri wake wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu ameikosoa miito ya kusitisha vita na badala yake kuitolea mwito jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja na Azerbaijan  akisisitiza kwamba hatua za huko nyuma za kusitisha vita zote zimeshindwa kufanikiwa kumaliza kile alichokiita ukaliaji wa mabavu wa Armenia wa eneo la Azerbaijan.

Türkei | PK | Mevlut Cavusoglu - Josep Borrell Fontelles in Ankara
Picha: picture-alliance/AA/C. Ozdel

Inaripotiwa kwamba nusu ya idadi ya watu wa Nagorno Karabakh wameachwa bila makaazi tangu yalipozuka mapigano hayo makali zaidi ya wiki moja iliyopita kati ya waasi wa  jimbo hilo lililojitenga na wanajeshi wa Azerbaijan. Armenia na Azerbaijan kwa miongo sasa ziko kwenye mgogoro kuhusu jimbo hilo linalokaliwa na jamii kubwa ya Warmenia ambalo kimsingi liko chini ya Azerbaijan.

Jimbo hilo lilijitenga na Azerbaijan katika miaka ya 1990 ilipotokea vita  vilivyosababisha kiasi watu 30,000 kuuwawa. Na pande zote mbili hivi sasa zimekataa kuitikia miito ya kusitisha mapigano huku kila mmoja akimtuhumu mwenzie  kwa kuanzisha vita hivi vipya vilivyoanza Septemna 27.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell ametowa mwito wa kufanyika mazungumzo mapya  kuhusu mgogoro huo akionya  juu ya uchochezi wa vyombo vya habari pamoja na uingiliaji wa nchi za kigeni.

Berg-Karabach Konflikt
Picha: David Ghahramanyan/NKR InfoCenter/PAN Photo/Reuters

Waziri mkuu wa Armenia Pashinian anailaumu Uturuki kwamba inaendeleza sera ya maangamizi dhidi ya Warmenia ili kurudisha himaya ya Uturuki katika ukanda huo.Iran ambayo inapakana na nchi zote mbili Armenia na Azerbaijan imeonya juu ya kuzuka vita vikubwa vya kikanda. Rais Rouhani ameonya kwamba vita katika jimbo la Nagorno Karabakh huenda vikachochea mapigano ya kieneo wakati vita hivyo vikiingia siku yake ya 11.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo