Marzouk: Assad umekwisha | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marzouk: Assad umekwisha

Rais wa Tunisia, Moncef Marzouk amemshauri rais Bashar Assad wa Syria kuachia madaraka wakati nafasi ya kufanya hivyo bado ipo kwa kuwa kuondoka kwake ni laazima akiwa mzima au mfu.

Rais Bashar al-Assad na mkewe Asma

Rais Bashar al-Assad na mkewe Asma

Rais Marzouk amesema njia peke aliyonayo Assad ni kuondoka kwa hiari na kwamba Tunisia itakuwa tayari kumpa hifadhi kama njia mojawapo ya kuleta amani nchini Syria.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la kiarabu la al-Hayat, rais Marzouk alisema Assad amekwisha na kwamba ataachia madaraka kwa nji yoyote ile. Pia alituma ujumbe kwa mataifa ya Urusi, China na Iran na kuwataka watumbue ukweli huo, na kwamba mataifa hayo hayana muda mrefu wa kuendelea kumkingia kifua Assad, bali wanachotakiwa kufanya ni kumshauri akabidhi madaraka kwa naibu wake.

Urusi, China na Iran, ambao ni washirika wakubwa wa rais Assad wamepinga juhudi za mataifa ya magahribi na yale ya kiarabu zinazolenga kulaani ukandamizaji unaofanya na utawala wa rais Assad dhidi ya kile kilichoanza kama mandamano ya amani kabla hayageuka kuwa mzozo unaotishia kuipeleka nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Gari la waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa likipita katika mitaa inayokaliwa na wafuasi wa Assad

Gari la waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa likipita katika mitaa inayokaliwa na wafuasi wa Assad

"Utakwenda kwa njia moja au nyingine," Marzouk alimuambia Assad na kuongeza kuwa "utakwenda ukiwa mzima au umekufa, hivyo ni bora kwako na kwa familia yako ukiondoka ukiwa mzima." Rais Marzouk alisema suluhisho la mgogoro wa Syria ni kufuata njia iliyofuatwa nchini Yemen ambapo rais Ali Abdullah Saleh alikabidhi madaraka kwa makamu wake baada ya kuhakikishiwa usalama wake chini ya mkataba uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa na mataifa ya kiarabu.

Aukandia mpango wa Annan
Amesema mpango wa amani wa Koffi Annan utashindwa kufikia malengo yake kwa kuwa idadi ya waangalizi mia tatu walioidhinishwa na Umoja wa Mataifa ni ndogo sana na hawataweza kusimamia kwa ufanisi usitishaji wa mapigano.

Shirika la haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London limesema Afisa moja wa Intelijensia aliuawa siku ya Jumanne katika kitongoji cha Barzeh kilichoko katika mji mkuu wa Damascus na televisheni ya Ikhbaria inayoegemea upande wa serikali iliripoti kuwa mlipuko wa bomu lilitogewa ndani ya gari ulitokea katika wilaya moja mjini Damascus na kujeruhi watu watatu na kuharibu majengo.

Ikhabaria iliwalaumu iliyowaita magaidi waliyo na silaha wanaolenga kuiangusha serikali ya rais Assad, kwa kutega bomu hilo. Umoja wa mataifa unasema mgorogoro huo uliyodumu kwa miezi kumi na mitatu sasa, umeua watu zaidi ya 9000, wakati utawala mjini Damascus unasema maafisa wake 2,600 nao wameuawa na waasi walioteka miji mbalimbali katika taifa hilo lenye wakaazi wapatao milioni 23.

Shirika la habari la Syria liliripoti siku ya Jumanne kuwa maafisa wa forodha walioko mpakani mwa Syria na Lebanon, wamekamata gari lililojazwa risasi na silaha mbalimbali zikiwemo bunduki za rasha rasha tatu, na roketi ya gruneti.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE\DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com