Marekani na Japan zaijadili Korea Kasakazini | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani na Japan zaijadili Korea Kasakazini

Marekani na Japan zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika ulinzi ili kukabiliana na kitisho cha Korea Kaskazini. Waziri wa ulinzi wa Marekani hakuweka wazi iwapo Marekani italazimika kuchukua hatua za kijeshi

Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis hakuweka wazi iwapo Marekani italazimika kuchukua hatua za kijeshi au kutofanya hivyo katika kukabiliana na kitisho hicho cha Korea Kaskazini wakati Tillerson alisema Marekani ingependelea majadiliano ya pamoja na taifa hilo la kikomunisti.  Viongozi wa Korea Kusini wanasema vita vingine katika rasi ya Korea si swali la kuuliza na hatua yoyote itakayochukuliwa lazima iridhiwe pia na nchi hiyo.

Hofu imezidi kuongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia  kitisho cha mashambulizi ya makombora ya masafa marefu pamoja na mipango inayohusaiana na silaha za nyukilia ya Korea Kaskazini. Korea Kaskazini imesema ilikuwa inafikiria  mipango ya kufyatua makombora kulenga kisiwa cha Guam kilichoko katika bahari ya Pasifiki kinachomilikiwa na Marekani ingawa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anaonekana kuchelewesha hatua hiyo. Kisiwa cha Guam ni eneo maalumu la kimkakati kiulinzi kwa Marekani.

Mkutano huo wa Washington kuhusiana na suala la usalama unafanyika huku Korea Kasakzini ikiwa tayari imefanya jaribio la makombora yenye uwezo wa kutoka bara moja kwenda jingine.

Vita vya maneno kati ya Marekani na Korea Kasakzini vimeongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kasakazini Kim Jong Un huku  Trump akiionya Korea Kaskazini kuwa itakabiliwa na hatua kali ambazo dunia haijawahi kuzishuhudia iwapo itaendelea na vitendo vyake vya uchokozi.

Korea Kaskazini yaonekana kuwa kitisho kwa Marekani na Japan

USA | Japans Verteidigungsminister Itsunori Onodera und Außenminister Taro Kono treffen auf US Außenminister Rex Tillerson und Verteidigungsminister James Mattis (REUTERS/J. Ernst)

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson, Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis na wenzao wa Japan katika mkutano kujadili usalama mjini Washington

Suala linalohusiana na kitisho cha Korea Kaskazini liligubika mazungumzo ya jana mjini Washington kati ya Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani  Rex Tillerson na wenzano wa Japan ambapo viongozi wote wa pande mbili walikubaliana kufanya kazi kwa ukaribu zaidi hususani katika suala hilo linalohusiana na Korea Kasakazini.

Waziri wa ulinzi wa Japan Itsunori Onodera alisema baada ya mazungumzo hayo kuwa  kuhusiana na kitisho cha Korea Kaskazini pande zote mbili zimekubaliana kuongeza mbinyo  pamoja na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi.

Japan imekuwa ikifikiria kuimarisha ulinzi katika kukabiliana na kitisho cha aina yoyote cha Korea Kasakazini.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alisisitiza kuwa Marekani inapendelea zaidi majadiliano ya pamoja na Korea Kaskazini lakini iwapo tu majadiliano hayo yatakuwa na maana.

Aliongeza kuwa juhudi  za Marekani ni kuwashawishi Korea Kasakzini kukubali majadiliano na kuwa majadiliano hayo yatapaswa  kuwa na mwisho mzuri kuliko majadiliano yaliyopita akitolea mfano wa hatua ya Korea Kasakazini kuvunja makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2005 yaliyoitaka nchi hiyo kuachana na mipango yake ya nyukilia.

Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu ulipitisha vikwazo vipya vikali dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni hatua ya kuikabana zaidi kuhusaiana na majaribio yake ya makombora hatua ambayo itaathiri mauzo ya nje ya bidhaa zitokanazo na maliasili za nchi hiyo.

China ambayo ni mshirika wa Korea Kasakzini kibiashara imeapa kutekeleza azimio hilo la Umoja wa Mataifa na tayari imeanza kuchukua hatua kuhusiana na vikwazo hivyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/dw

Mhariri: Elizabeth Shoo

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com