1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na mpango mpya wa wahamiaji

9 Novemba 2018

Utawala wa Rais Donald Trump umesema kwamba utawanyima hifadhi wahamiaji ambao wataingia nchini Marekani kinyume na sheria, na kutumia nguvu za rais za usalama wa taifa kuilinda mipaka

https://p.dw.com/p/37wRF
Flüchtlinge US-Grenze bei Tijuana
Picha: Getty Images/D. McNew

Mikakati hiyo inapania kuwachuja wanaotafuta hifadhi kupitia mipaka halali inayotambuliwa kwa uamuzi wa haraka, badala ya wao kujaribu kuvuuka kupitia mpaka uliopo kilomita 3,200. Hata hivyo mipaka ya kuingia tayari inashuhudia foleni ndefu, suala linalowalazimu maafisa wa uhamiaji kuwataka baadhi ya wahamiaji kurejea baadaye kuleta maombi yao.

Hatua hiyo imechangiwa na misafara ya wahamiaji wa Amerika ya Kati ambao wanajaribu kuingia Marekani kwa miguu, lakini pia itawaathiri wote watakaopatikana wakivuuka mipaka kinyume na sheria. Haijabainika iwapo wahamiaji walioko kwenye msafara, wengi waliotoroka vita katika nchi zao wanapanga kuvuuka kinyume na sheria ama la.

Donald Trump spricht über Einwanderungspolitik
Picha: picture-alliance/C. Kleponis

Kanuni hizo zitatajwa kwenye tangazo linalotarajiwa kutolewa leo na Rais Donald Trump. Maafisa wanaohudumu katika serikali ya Marekani ambao walizungumza na shirika la habari la Associated Press, na ambao hawakutaka kutajwa majina, wamesema Rais Trump atatumia nguvu alizotumia kutekeleza marufuku ya usafiri yaliyoidhinishwa na Mahakama ya Juu zaidi. 

Kadhalika wamesema wahamiaji watakaonyimwa hifadhi watapewa ulinzi sawa iwapo wataogopa kurejea katika nchi zao, lakini watakabiliwa na vizingiti vigumu zaidi. Kukabili uhamiaji limekuwa suala kuu kwa Rais Trump, ambaye amelizungumzia kwa upana hadi kuelekea katika uchaguzi wa katikati ya muhula, na kutoa kashfa dhidi ya ya misafara ambayo iko maili kadhaa kutoka kwenye mpaka wa Marekani.

Mexiko Tijuana Migranten-Konvoi erreicht US-Grenze
Picha: Getty Images/D. McNew

Hajalizungumzia suala hilo tangu uchaguzi huo lakini ameyatuma majeshi mpakani. Vile vile Trump alipendekeza kwamba atafutilia mbali haki za kupewa uraia kwa watoto wanaozaliwa na watu wasiokuwa raia wa Marekani nchini humo. Hata hivyo suala hilo halijatajwa kwenye kanuni zilizotolewa jana kuhusu wahamiaji wanaotafuta hifadhi.

Sehemu ya Sheria ya Uhamiaji na Uraia inasema kwamba mhamiaji anaruhusiwa kutoa maombi ya hadi mwaka mmoja baada ya kuwasili Marekani, na haijalishi ni vipi walivyoingia nchini humo, kinyume na sheria au kupitia mpakani. Wahamiaji ambao wamekuwa wakivuka mipaka kinyume na sheria hukamatwa na baadaye kuomba hifadhi au ulinzi. Kwa ujumla ni asilimia 20 pekee ya wahamiaji wanaotuma maombi hukubaliwa.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Mohammed Khelef