Marekani kutuma wanajeshi Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Marekani yarudi Somalia

Marekani kutuma wanajeshi Somalia

Marekani iliondoka Somalia baada ya mwaka 1993 wakati helikopta zake mbili zilipodunguliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu na maiti za wanajeshi wake kuburuzwa na kupitishwa katika mitaa ya mji huo wa Mogadishu.

US Soldaten in Somalia 1994 (picture alliance/AP Images/ Moore)

Kikosi cha Marekani 1994 katika uwanja wa ndege Mogadishu

Marekani iliondoka Somalia baada ya mwaka 1993 wakati helikopta zake mbili zilipodunguliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu na maiti za wanajeshi wake kuburuzwa na kupitishwa katika mitaa ya mji huo wa Mogadishu. Hata wakati huu serikali kuu dhaifu ya Somalia inapambana kujiweka sawa yenyewe baada ya kushuhudia ghasia na vita vilivyoanza muda mfupi baada ya kuangushwa madarakani dikteta Siad Barre mwaka 1991.

Kamandi ya kijeshi ya Marekani barani Afrika siku ya Ijumaa ilisema kwamba kupelekwa kikosi cha wanajeshi 40 wa Marekani Somalia kunanuiwa kutoa huduma ya mafunzo ya kiusafiri kwa jeshi la Somalia ambalo linapambana dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa kundi la Al-Shabab, kundi lililozuka kutokana na miaka kadhaa ya mgogoro uliochochewa na  wababe wa kivita. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Marekani imewahi kupeleka idadi ndogo ya kikosi maalum kwa ajili ya shughuli maalum pamoja na washauri wa kupambana na ugaidi katika nchi hiyo ya Somalia na rais Donald Trump siku za karibuni aliidhinisha hatua ya kutanua dhima ya jeshi la Marekani katika taifa hilo la Somalia.

Afrika AMISOM Symbolbild African Standby Dorce (Reuters/A. Wiegmann)

Wanajeshi wa AMISOM

Dhima ya kikosi hicho ni pamoja na kuchukua hatua za kutumia nguvu zaidi za kijeshi na haa mashambulio ya angani dhidi ya Al Shabab pamoja na kuliweka eneo la upande wa Kusini mwa Somalia katika orodha ya maeneo hatari. Rais mpya wa Somalia ambaye anauraia wa nchi mbili Somalia na Marekani Mohammed Abdullahi Mohammed wiki iliyopita alitangaza operesheni mpya dhidi ya kundi hilo la itikadi kali ambalo linaendesha shughuli zake nchini Somalia lakini pia linabeba dhamana ya mashambulizi mengi makubwa katika eneo zima la Afrika Mashariki ikiwemo shambulio kubwa lililouwa watu 148 katika chuo kikuu cha mjini Garissa kwenye nchi jirani ya Kenya Aprili mwaka 2015.

Wiki hii kundi hilo lilitangaza kwamba kuenea kwa mashambulio yaliyosababisha mauaji hivi karibuni mjini Mogadishu na kwengineko ni hatua ya kujibu mara dufu mpango wa Donald Trump wa kuidhinisha kutanua juhudi za kijeshi za Marekani.Ikumbukwe kwamba Al-Shabab ni kundi lililotimuliwa mjini Mogadishu miaka mingi iliyopita na kikosi cha jeshi la taifa likisaidiwa na kikosi kikubwa cha Umoja wa Afrika lakini kundi hilo bado linashikilia maeneo kadhaa ya vijijini.

Kenia Nairobi Besuch Somalischer Präsident (picture-alliance/AP Images/K. Senosi)

Kushoto-RaisMohamed Abdullahi wa Somalia na Uhuru Kenyatta wa Kenya

Wakati huohuo kuna kundi ambalo kwa upande mwingine limezuka na limekula kiapo kuliunga mkono kundi linalojiita Dola la Kiislamu kaskazini mwa Somalia.Jshi la Somalia linazidi kukabiliwa na shinikizo la kulitaka liwe tayari kuchukua dhamana ya kuendesha kikamilifu shughuli za usalama wa taifa hilo wakati ambapo wanajeshi 22,000 wa Umoja wa Afrika wakijiandaa kuondoka nchini humo kufikia mwishoni mwa mwaka 2020. Kimsingi kikosi hicho cha AU kitaanza rasmi kuondoka mwaka 2018 amesema Jenerali mkuu wa jeshi maalum la Marekani ThomasWaldHauser.

Mwandishi: Yusuf Saumu/AP

Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com