Marekani ina matumaini ya kufikia makubaliano na Iran
16 Aprili 2026
Marekani imesema ina matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano na Iran huku ikiendelea kujadili uwezekano wa duru ya pili ya mazungumzo ya amani, ambayo huenda yakafanyika nchini Pakistan.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mazungumzo hayo yanaweza kufanyika katika mji mkuu Islamabad, kufuatia juhudi mpya za kidiplomasia zinazolenga kumaliza mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel.
Ujumbe wa Pakistan umefika Tehran ukiwasilisha ujumbe mpya kutoka Washington, baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo kushindwa wiki iliyopita.
Wakati huo huo, Israel imesisitiza malengo yake ya kuondoa uwezo wa Iran wa kurutubisha urani na kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, eneo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani.
Huku mvutano ukiongezeka, Marekani imeongeza vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran, wakati Tehran ikionya kuwa haitaruhusu meli yoyote kupita katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman au Bahari ya Shamu endapo vizuizi havitaondolewa.