Marais 35 kuhudhuria mkutano wa usalama mjini Munich | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marais 35 kuhudhuria mkutano wa usalama mjini Munich

Mkutano wa masuala ya usalama unaanza hivi leo katika mji wa Munich ukihudhuriwa na viongozi kutoka kila pembe ya dunia kwa lengo la kujadili namna ya kuleta amani wakati kunashuhudiwa migogoro sehemu mbalimbali duniani.

Wolfgang Ischinger Sicherheitskonferenz

Mwenyekiti wa mkutano wa masuala ya usalama duniani Wolfgang Ischinger,

Mji wa Munich ulioko kusini mwa Ujerumani utakuwakutanisha zaidi ya marais 35 pamoja viongozi wakuu kutoka kila pembe ya dunia akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau.

Nchi nyengine zinatuma mawaziri kama wawakilishi wao katika mkutano huo wa kila mwaka wa masuala ya usalama duniani kama vile waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, Wang Yi wa China na Mohammad Javad Zarif wa Iran.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper na mwenyekiti  mtendaji wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg, pia wako kwenye orodha ya watakaohudhuria mkutano huo.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo, mwenyekiti wa mkutano huo, Wolfgang Ischinger, amesema kuwa amesikitishwa na hatua ya jamii ya kimataifa kukosa kupata suluhu ya mgogoro unaoukumba Syria kwa sasa. Ischinger pia ameweka wazi kuwa mpango wa amani ambao mazungumzo yake yalifanyika mjini Berlin pia umefeli.

"Kuna migogoro na matukio ya kutisha, mengine yenye uzito zaidi yenye kutukabili ambayo mtu hawezi hata kufikiria yanaweza kutokea", alisema Wolfgang Ischinger.

Migogoro inayoendelea duniani ni changamoto kwa usalama

Migogoro na vita vinavyoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali duniani inaonyesha jinsi kazi kubwa inayowakabili wanaohudhuria mkutano huo ambao utaendelea hadi Jumapili.

Kando na kujadili namna ya kutatua migogoro duniani, mkutano huo pia huenda ukazungumzia suala la mvutano na kutoelewana katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Mvutano huo unajadiliwa wakati huu ambapo Rais Macron wa Ufaransa anatia mkazo Ulaya kuwa huru zaidi badala ya kutegemea sana Marekani.

Wakati huo huo, Spika wa bunge la Congress Nancy Pelosi ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Donald Trump pia anatarajiwa kuwepo kwenye mkutano huo.

Kuwepo kwake kutamaanisha kuwa wakosoaji na vilevile wanaomuunga rais huyo wa Marekani watawakilishwa kwenye jukwaa hilo la kimataifa.

Maafisa wa usalama 3,900 wamewekwa ili kushika doria wakati wa mkutano huo.

Vyanzo DPA