1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan Kusini

Mapigano Sudan Kusini yaua zaidi ya watu 50

29 Januari 2024

Zaidi ya watu 50 wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa kwenye mashambulizi yaliofanyika kwenye eneo la mpaka kati ya Sudan Kusini na Sudan.

https://p.dw.com/p/4bnZB
Wapiganaji wa Sudan
Picha ikiwaonyesha wapiganaji wa SudanPicha: Camera4/Jim/imago images

Hili ni tukio baya zaidi kushuhudiwa eneo hilo katika mfululizo wa mashambulizi yanayohusishwa na mgogoro wa mipaka wa tangu mwaka 2021 kati ya mataifa hayo jirani.

Taarifa hii imetolewa leo na afisa mmoja wa eneo hilo ambaye amesema kuwa watu 52 waliuawa kufuatia mapigano katika eneo linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Bulis Koch, waziri wa habari wa eneo la Abyei amesema kundi la vijana wenye silaha kutoka Jimbo la Warrap huko Sudan Kusini walifanya uvamizi katika mkoa jirani wa Abyei, ambao ni eneo lenye utajiri wa mafuta linalosimamiwa kwa pamoja na mataifa hayo mawili jirani ambayo kila mmoja linadai ni sehemu yake.

Koch ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu 52, wakiwemo wanawake, watoto na maafisa wa polisi, wameuawa katika mashambulizi ya Jumamosi huku watu wengine 64 wakijeruhiwa. Afisa huyo amesema wameweka amri ya kutotoka nje kutokana na hali mbaya ya usalama iliyoibua hofu.

Afisa wa kikosi cha Umoja wa Mataifa auawa

Kikosi cha UNISFA huko Abyei
Wanajeshi wa kulinda amani wa Kikosi cha muda cha Umoja wa Mataifa huko Abyei (UNISFA)Picha: Albert Gonzales Farran/AFP/Getty Images

Kikosi cha muda cha Umoja wa Mataifa huko Abyei (UNISFA) kimesema hapo jana kuwa askari wa kikosi hicho cha kulinda amani raia wa Ghana aliuawa baada ya kushambuliwa kwa kituo alichokuwamo kwenye mji wa Agok.

Kwa mujibu wa Koch, mamia ya raia waliokimbia makazi yao wametafuta hifadhi kwenye kituo hicho cha UNISFA. William Wol, waziri wa habari wa Jimbo la Warrap, amesema serikali yake itafanya uchunguzi wa pamoja na utawala wa mkoa wa Abyei.

Soma pia: Mapigano mapya yazuka kusini mwa Sudan

Kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara huko Abyei kati ya makundi hasimu ya kabila la Dinka kuhusiana na eneo la mpaka wa kiutawala ambao kwa kiasi fulani ni chanzo cha mapato kutokana na ukusanyaji wa kodi.

Eneo la Abyei linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini
Eneo la Abyei linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan Kusini

Bulis Koch, waziri wa habari wa eneo hilo la Abyei amesema vijana wa Dinka kutoka Warrap na kiongozi wa vikosi vya waasi wa kabila la Nuer ndiyo waliotekeleza mashambulizi dhidi ya jamii ya Dinkas na Nuers huko Abyei.

Kati ya mwaka 2013 na 2018, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini  ambavyo kwa kiasi kikubwa ni vyenye misingi ya kikabila kati ya Dinkas na Nuers, tayari vimesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu.

Tangu wakati huo, mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi ya watu wenye silaha yameendelea kusababisha maafa makubwa eneo hilo ikiwa ni pamoja na vifo na kuwahamisha raia. Mapigano ya mwezi Novemba mwaka jana huko Abyei yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 32.

(Chanzo: RTRE)