Maoni ya wahariri juu ya Rais Rouhani | Magazetini | DW | 26.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya Rais Rouhani

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya ziara ya Rais wa Iran Rouhani barani Ulaya, mazungumzo juu ya kuutaua mgogoro wa Syria na pia wanatoa maoni juu ya tofauti kubwa kati ya tajiri na masikini

Rais wa Iran Hassan Rouhani na Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi

Rais wa Iran Hassan Rouhani na Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi

Katika maoni yake gazeti la "Neues Deutschland" linaitilia maanani ziara ya Rais wa Iran Hassan Rouhani nchini Italia na Ufaransa. Mhariri wa gazeti hilo anasema lengo la ziara hiyo ni kuurejesha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi yake na nchi za Ulaya.

Mhariri wa "Neues Deutschland" anasema Rais Rouhani hakutaka kusubiri. Mara tu baada ya vikwazo kuondolewa amekuja Ulaya na orodha ndefu ya mahitaji muhimu kwa uchumi wa nchi yake. Pamoja na hayo inapasa kusisitiza kwamba kila mkataba wa kibiashara baina ya Iran na nchi za magharibi, unauimarisha mkataba wa nyuklia ambao Iran imeufikia na mataifa makubwa sita .

Gazeti la "Handelsblatt" linazungumzia juu ya mkutano unatotarajiwa kufanyika Ijumaa ijayo mjini Geneva kwa lengo la kuutatua mgogoro wa nchini Syria.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba mahasimu wakubwa watakutana ili kujaribu kuleta suluhisho la kisiasa. Mhariri huyo anasema hii ni mara ya tatu, kwamba Umoja wa Mataifa unajaribu kuzileta pamoja pande zinazohusika na mgogoro wa nchini Syria. Mikutano ya hapo awali ilishindikana, na hata huu wa tatu umeonyesha mashaka.

Mhariri wa "Handelsblatt"anasema mpaka sasa haijajulikana ni nani atakaeuwakilisha upande wa upinzani, wakati damu inaendelea kumwagika kwenye uwanja wa mapambano.

Bei ya mafuta yazidi kuporomoka

Bei ya mafuta yazidi kuanguka

Bei ya mafuta yazidi kuanguka

Mhariri wa gazeti la "Straubuinger Tagblatt" anasema nchi zinazouza mafuta sasa zinakabiliwa na matatizo makubwa kutokana na bei ya mafuta kuanguka sana. Mhariri wa gazeti hilo anasema ingawa kushuka kwa ya mafuta ni habari nzuri kwa wateja wa kawaida, biashara baina ya nchi hizo na kampuni za Ujerumani inaathirika kwa kiwango kikubwa.

Mhariri huyo anasema inapasa kutambua kwamba wateja hao wa kawaida ni muhimu katika kuustawisha uchumi.

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linatahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka tofauti baina ya tajiri na masikini. Mhariri wa gazeti hilo anashauri haja ya kuzitilia maanani tofauti hizo kisiasa na kijamii

. Anasema pengo hilo linalosababisha kutengwa kwa mabaka fulani ya jamii litazua athari. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linataka hatua zichukuliwe la sivyo, linasema tofauti hizo zitaendelea kuwa kubwa katika miaka ijayo. Tofauti hizo zitajenga mazingira ambapo itakuwa vigumu kwa watu wenye ustadi mdogo kupata ajira.

Katika hali hiyo anasema mhariri wa gazeti hilo watu watahisi kuwa wamepoteza hadhi ya kibidamu na kutumbukia katika umasikini.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com