Maoni: Ushindi wa mwisho wa Mugabe | Matukio ya Afrika | DW | 22.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maoni: Ushindi wa mwisho wa Mugabe

Kwa mara nyingine tena, Robert Mugabe ameapishwa kuwa rais wa Zimbabwe. Licha ya kuwa na miaka 89 sasa, Mugabe haonyeshi dalili yoyote ya kuchoshwa na siasa. Mwandishi wetu Claus Stäcker anashangazwa na jambo hilo.

Mkuu wa idhaa za Kiafrika, Claus Stäcker

Mkuu wa idhaa za Kiafrika, Claus Stäcker

Mugabe ni bingwa katika nyanja zote. Licha ya kuwa mzee anawashinda wote kwa ujanja: wananchi wake, jumuiya ya maendeleo ya nchi Kusini mwa Afrika SADC, Umoja wa Afrika na mataifa ya Magharibi. Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 89 ni rais mpya na wazamani wa Zimbabwe. Kuapishwa kwake kumesimika nafasi yake kwenye kiti cha urais na kumpa nguvu kubwa ambayo hakuwa nayo katika miaka 13 iliyopita.

Mwaka 2000, yalipofanyika mabadiliko ya katiba ya mwisho yanayoweza kuelezewa kuwa ya kidemokrasia, wananchi walipinga mpango wa Mugabe wa kutanua madaraka yake. Hilo likawa onyo kwake. Mtikisiko wa kwanza ulikuja mwaka 2002, pale ambapo alichaguliwa tena kuwa rais katika uchaguzi ambao ulikuwa na wizi wa kura wa wazi wazi. Lakini hakuna kilichotokea, Mugabe alibakia madarakani.

Wizi wa kura kwa miaka 11

Mwaka 2008 mambo yakawa mabaya zaidi: Hata waangalizi wa uchaguzi hawakuweza kubisha kuwa raia wengi hawakukichagua chama tawala cha ZANU-PF. Baada ya vuta nikuvute na propaganda nyingi Mugabe alifanikiwa kubaki madarakani.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu yameonyesha kuwa Mugabe amepata asilimia 61 ya kura na kumfanya aonekane kama kiongozi aliyechaguliwa kihalali. Sauti chache tu kutoka Afrika zimekosoa uchaguzi huo. Orodha ya wageni waalikwa katika sherehe za kumwapisha Mugabe zinaonyesha wazi nchi gani zinamuunga mkono na zipi zinazopingana naye.

Rais Ian Khama wa Botswana anaelezwa kuwa adui mkubwa wa Mugabe na hivyo hakufika leo. Kwa upande mwingine, Afrika Kusini ilimtuma makamu wake wa rais kushuhudia kuapishwa kwa Mugabe. Kwa namna hiyo, raisJacob Zuma anataka kuashiria kuwa anaelewana na Mugabe lakini hataki kuhusishwa naye kwa karibu zaidi.

Kushindwa kwa demokrasia

Wachambuzi wa nchi za Magharibi wanashangaa kuona namna ambavyo Mugabe anaungwa mkono na watu wengi barani Afrika. Inaelekea kuwa nusu ya bara la Afrika linafurahia kisirisiri pale ambapo Mugabe anaanza kugomba juu ya wale anaowaita walowezi wa kikoloni. Hata wasomi wanakiri kwamba hakuna anayethubutu kusema mambo hayo wazi wazi kama mzee huyu.

Lakini mara nyingi inasahaulika kwamba katika safari yake ndefu ya kuiletea uhuru Zimbabwe na kisha kuiongoza nchi hiyo, Mugabe amewaweka kando wagombea uhuru wengi waliopambana pamoja naye. Mwisho wa siku amebakia shujaa mmoja tu katika historia ya Zimbabwe: Mugabe mwenyewe.

Huenda sababu moja ya Mugabe bado kuwa madarakani ni udhaifu wa chama kikuu cha upinzani MDC. Chama hicho hakitoi njia mbadala kwa mtindo wa utawla wa Mugabe. Inaweza kusemwa kuwa Mugabe ni bingwa katika nyanja zote, mshawishi aliyebobea na zamani alikuwa shujaa. Lakini Mugabe si rais halali. Kushinda kwake ni kushindwa kwa demokrasia barani Afrika

Mwandishi: Claus Stäcker

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza