Maoni: Amani ya Ethiopia yavutwa kwa ndoano | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

ETHIOPIA

Maoni: Amani ya Ethiopia yavutwa kwa ndoano

Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Abiyi anataka hatimaye kutambua makubaliano ya amani ya muda mrefu na Eritrea baada ya miaka 20, hiyo ni habari njema lakini bado ni mapema mno kusherehekea, anasema Ludger Schadomsky.

Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Dr. Abiy Ahmed (Oromia Government Communication Affairs Bureau)

Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Dr. Abiy Ahmed

Watu nchini Ethiopia karibuni watapata kizunguzungu kutokana na kasi ya utendaji kazi ya waziri mkuu mpya Abiy. Kabla hata miezi miwili haijamalizika vizuri, waziri mkuu huyo ameshachukua hatua za mageuzi zinazowazungusha vichwa watawala wa hapo zamani waliokwishaingiwa kutu.

Maelfu ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa, mdahalo wa kuleta maridhiano unafanyika baina ya serikali na wapinzani na hali ya hatari iliondolewa mapema.

Na sasa, baada ya miaka mingi ya mvutano wa kisiasa, Ethiopia inataka kuitambua hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague ya mwaka 2002. Mahakama hiyo iliipa haki Eritrea juu ya sehemu ya mpaka wake na Ethiopia.

Äthiopien Addis Abeba Premierminister Abiy Ahmed (Reuters/T. Negeri)

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Baada ya hatua hizo watu nchini Ethiopia wanajiuliza je, nini kinafuata? Je, ni mapatano ya amani juu ya matumizi ya maji ya mto Nile baina yake na jirani yake Misri?

Katika hotuba yake ya kuingia madarakani waziri mkuu mpya wa Ethiopia alitangaza hatua za amani na nchi jirani yake Eritrea. Lakini kasi aliyoitumia kuzitekeleza hatua hizo ni ya kushangaza.

Hatua ya kukiri kwa haraka iliyochukuliwa na Ethiopia, kimsingi ni ushindi kwa adui yake mkubwa Eritrea kuhusu mgogoro wa mpaka. Ndiyo kusema sehemu zilizopendekezwa na tume ya usimamizi ya Eritrea, ikiwa pamoja na ile ambayo imekuwa inayozozaniwa ya Badme, zitapaswa zirudishwe kwa Eritrea. Ethiopia itapaswa ikabidhi sehemu hizo. Lakini swali ni je, Eritrea iko tayari kuukubali mkono huo wa amani? Inasemekana kuwa utawala wa Eritrea haujapendezwa na mabadiliko ya kisiasa ya nchini Ehtiopia.

Ludger Schadomsky wa DW

Ludger Schadomsky wa DW

Tangu kutolewa kwa uamuzi na mahakama ya kimataifa juu ya mgogoro wa mpaka wake na Ethiopia, dikteta wa Eritrea Isaias Afwerki amekuwa anazungumzia anachoita hali ya kutokuwepo amani wala vita! 

Hali ya kuwa tayari kivita inauwezesha utawala wa Afwerki kuendeleza udhalimu na uongozi wake unaosababisha maalfu kwa maalfu ya vijana waikimbie nchi yao. Siasa ya maridhiano kutoka Ethiopia itaufanya utawala wa Afwerki ushindwe kuitekeleza sera ya kuwaandikisha vijana jeshini kwa nguvu, siasa ambayo imedhibiti maisha ya kila raia wa Eritrea katika muda wa miongo miwili iliyopita na ambayo imekuwa inahalalisha utawala wa kiongozi wa nchi hiyo Afwerki.

Mpaka sasa Eritrea haijatoa jibu rasmi kwa Ethiopia. Na kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni kiongozi wa Eritrea amekataa usuluhishi wa kidiplomasia wa Saudi Arabia. Mkakati wa rais Afwerki wa kutetea uwepo wake wa kisiasa kwa njia hiyo unaweza kuyavunja matumaini ya kuleta amani kwenye pembe ya Afrika ambako kwa miaka mingi imekuwa sehemu isiyokuwa na utulivu. Kutokana na hali hiyo ni mapema mno kushanigilia kwa sauti kubwa nchini Ethiopia kwenyewe na pia nchini Eritrea.

Mwandhishi: Zainab Aziz/ Schadomsky, Ludger

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com