Malaysia: Je, mkutano wa ASEAN unaweza kuleta amani?
26 Oktoba 2025
Mvutano wa mpakani kati ya Thailand na Cambodia pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar vitakuwa mada kuu za mjadala katika mkutano ujao wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) utakaofanyika katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur.
Malaysia, ambayo kwa sasa inashikilia uenyekiti wa mzunguko wa ASEAN, itapokea zaidi ya wakuu wa nchi 30 katika mkutano huo wa Oktoba 26–28, akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye anatarajiwa kushuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya Thailand na Cambodia.
Majirani hao wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa mpaka unaodumu kwa zaidi ya karne moja.
Mvutano katika eneo la mpaka wa Thailand na Cambodia ulizuka kuwa mapigano makubwa mwezi Julai, ambapo watu angalau 43 waliuawa na raia 300,000 walikimbia makazi yao katika kipindi cha siku tano za mapigano.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Malaysia, China, na Marekani yalianza kutekelezwa Julai 29Mkutano wa ASEAN: Viongozi kujadili mvutano wa ushawishi kati ya China na Marekani.
Hata hivyo, licha ya makubaliano ya amani, mvutano bado umeendelea kati ya mataifa hayo jirani. Thailand imeituhumu Cambodia kwa kuweka mabomu ya ardhini katika baadhi ya maeneo ya mpaka wao wa pamoja, ikidai kwamba wanajeshi kadhaa wa Thailand wamejeruhiwa vibaya na vilipuzi hivyo tangu mwezi Julai.
Cambodia imekanusha tuhuma hizo, ikisema kwamba baadhi ya wanajeshi wa Thailand walikanyaga mabomu yaliyosalia kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa, ambavyo vimeifanya Cambodia kuwa miongoni mwa nchi zilizo na mabomu mengi zaidi duniani.
Marekani yasukuma mpango wa amani ya kudumu
Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kusimamia kutiwa saini kwa makubaliano rasmi ya amani ya kudumu kati ya Thailand na Cambodia.
Awali, Trump alitishia kuongeza ushuru wa kibiashara kwa mataifa yote mawili endapo mapigano yangeliendelea. Hata hivyo, baada ya pande hizo mbili kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Julai, Thailand na Cambodia zilipata punguzo la ushuru hadi asilimia 19.
Mark S. Cogan, profesa mshiriki wa masomo ya amani na migogoro katika Chuo Kikuu cha Kansai Gaidai, Osaka, Japan, alisema Kuala Lumpur pia imekuwa ikitegemea uingiliaji wa Marekani ili kuimarisha shinikizo kwa Bangkok na Phnom Penh, kama nyongeza ya juhudi zake za kutatua mgogoro huo.
"Malaysia imeipa Marekani na Trump nafasi kubwa katika mazungumzo ya Thailand na Cambodia, ikitumaini kuwa shinikizo la kisiasa kutoka Washington pamoja na vivutio vya kiuchumi vitatosha kuzifanya pande zote mbili kuheshimu makubaliano yatakayotiwa saini,” Cogan aliambia DW.
"Diplomasia ya Malaysia imekuwa nguzo muhimu katika mazungumzo haya, na makubaliano hayo mapya yanatarajiwa kuitwa Makubaliano ya Kuala Lumpur, yakilenga kuhakikisha pande zote mbili zinachukua hatua za kudumisha usitishaji wa mapigano.”
Je, ASEAN inaweza kupata suluhisho la amani nchini Myanmar?
Juhudi za kidiplomasia za Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) katika kutatua mgogoro wa Myanmar hadi sasa zimeonekana kushindikana.
Myanmar imekuwa katika hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mapinduzi ya kijeshi ya Februari 2021 yalipoiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia iliyoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, na kuchochea uasi wa kitaifa.
Tangu mapinduzi hayo, zaidi ya watu milioni 3.5 wamekimbia makazi yao na maelfu wameuawa. Mchanganyiko wa makundi ya upinzani, vikosi vya ulinzi vya wananchi, na makundi ya waasi wa kikabila umeendelea kupigana dhidi ya utawala wa kijeshi.
Mwezi Julai, madaraka yalihamishwa kwa serikali ya kiraia ya mpito, ambayo inapanga kufanya uchaguzi kuanzia Desemba 28.
Uchaguzi wa Myanmar 2025
Kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Jenerali Min Aung Hlaing, ambaye kwa sasa anakaimu urais, ametaja uchaguzi ujao kama njia ya upatanisho wa kitaifa, licha ya kukiri kuwa hautafanyika kote nchini kutokana na mapigano yanayoendelea.
Wachunguzi wa kimataifa na mashirika ya haki za binadamu wameupuuza uchaguzi huo wakisema ni mbinu ya kuhalalisha kuendelea kwa utawala wa kijeshi nchini humo.
Serikali ya Malaysia imesisitiza kuwa kipaumbele nchini Myanmar kinapaswa kuwa kumaliza machafuko na kujenga amani badala ya kufanyika kwa uchaguzi. Hata hivyo, wajumbe wa mkutano wa kilele wa ASEAN wanatarajiwa kujadili suala la kutuma waangalizi kufuatilia uchaguzi wa Desemba.
"Malaysia italazimika kueleza jinsi ASEAN itakavyoshughulikia uchaguzi wa Desemba nchini Myanmar, kwa kuwa jeshi limekaribisha waangalizi wachache, lakini sidhani kama ASEAN itawatuma,” alisema Sharon Seah, mhadhiri mwandamizi wa taasisi ya ISEAS–Yusof Ishak huko Singapore.
ASEAN bado yapambana kutekeleza mpango wa Myanmar
Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) imekuwa ikihangaika kutekeleza kile kinachoitwa *Mpango wa Mambo Matano* uliokubaliwa na viongozi wa eneo hilo mwaka 2021 ili kushughulikia mgogoro wa Myanmar. Mpango huo unajumuisha kusitisha machafuko, upatanishi, kuimarisha mazungumzo, kutoa misaada ya kibinadamu, na ziara ya mjumbe maalum wa ASEAN nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Mohamad Hasan, alisema Ijumaa kwamba utekelezaji wa mpango huo si jambo gumu, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters. Aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa maafisa wakuu wa ASEAN kwamba Myanmar imesihiwa kutekeleza mpango huo na kuruhusu usambazaji wa misaada. Hata hivyo, jeshi la Myanmar na ASEAN yenyewe zimekosolewa kwa kushindwa kuutekeleza ipasavyo.
Viongozi wa kijeshi wa Myanmar wamezuiwa kuhudhuria mikutano ya ngazi ya juu ya ASEAN kutokana na kushindwa kutekeleza mpango huo wa mambo matano. "Nadhani baada ya mkutano huu, [Malaysia] itaweka masharti zaidi kwa Myanmar,” alisema Sharon Seah.
Kwa upande wake, Profesa Mark Cogan alisema mitazamo tofauti ndani ya ASEAN kuhusu Myanmar ndiyo inayokwamisha maendeleo ya amani. Hakutarajia mafanikio makubwa kuhusu suluhisho la kudumu nchini humo. "Ni vigumu kuona hali ikiboreka wakati ASEAN imegawanyika — baadhi ya nchi zikitaka kuitenga Myanmar, na nyingine zikisisitiza ushirikiano,” alisema.
"Malaysia imekuwa ikijaribu kusawazisha msimamo wake, lakini sasa imeanza kuhoji sera ya muda mrefu ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi wanachama — sera ambayo imeidhoofisha ASEAN wakati wa mgogoro huu. Isipokuwa jumuiya ivunje utamaduni huo hivi karibuni, hakuna matumaini makubwa kwamba mkutano huu utazaa matokeo chanya.”
Hatua muhimu katika upanuzi wa ASEAN
Licha ya wasiwasi kuhusu kama migogoro ndani ya ASEAN inaweza kutatuliwa, jambo moja chanya kwa jumuiya hiyo ya kikanda ni kwamba itakaribisha mwanachama mpya Jumapili hii.
Kwa sasa, ASEAN ina wanachama kamili 10 wakiwemo Thailand, Laos, Vietnam, Cambodia, Myanmar, Malaysia, Singapore, Indonesia, Brunei, na Ufilipino. Timor-Leste itakuwa mwanachama wa 11 wa kudumu wa jumuiya hiyo, baada ya kuwasilisha ombi la uanachama kwa mara ya kwanza mwaka 2011.