Makahama ya Kenya yakataa kusitisha 16% ya kodi ya mafuta | Matukio ya Afrika | DW | 04.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Makahama ya Kenya yakataa kusitisha 16% ya kodi ya mafuta

Inaoenekana Wakenya watalazimika kuendelea kukaza mikanda yao kufuatia kutekelezwa kwa kodi ya asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta. Hii ni baada ya mahakama kuu kukataa kusitisha utekelezaji wake kwa muda, licha ya kuitaja kesi hiyo kuwa ya dharura na kuagiza isikilizwe Jumatatu ijayo.

Sikiliza sauti 02:55

Hayo yanajiri baada ya kesi mbili kuwasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtata na Chama cha Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi nchini Kenya kwa lengo la kutaka uamuzi huo ubatilishwe kwa kukiuka katiba. 

Uamuzi wa Jaji Chacha Mwita ni pigo kwa Wakenya wengi ambao walikuwa na matumaini kuwa wangepata nafuu. Mahakama imesema kuwa pande zote zinastahili kusikizwa kabla ya uamuzi huo kutolewa, ingawa haujulikani utatolewa lini. 

Mafuta ni uti wa mgongo kwenye sekta zote nchini Kenya, na sasa athari ya kuongezwa kwake kodi kunapandisha gharama ya maisha, huku bei za bidhaa za msingi zikiongezeka. Kodi hiyo inalenga kuchangisha shilingi bilioni 30 kwenye bajeti ya shilingi trilioni tatu ya mwaka 2018/2019. 

Hayo yanajiri licha ya bunge kuagiza kusitishwa kutekeleza kwa ongezeko hilo la kodi. Kuongeza msumari mmoto kwenye donda bichi, wasafarishaji wa mafuta hayo wamegoma kuyasambaza, hali ambayo huenda ikasababisha uhaba wake. Baadhi ya wenye magari ya usafirishaji wameanza kuongeza nauli zao. Aidha baadhi yao wanatisha kugoma iwapo rais hataingilia kati suala hilo.

Ruto aamini serikali itatilia manani kilio cha Wakenya

Ongezeko la kodi linamaanisha kuwa Wakenya wanaotumia usafiri wa umma sasa wanalazimika kulipia asilimia 20 zaidi ya nauli. Bei mpya ya mafuta ya taa ni shilingi 97, petroli shilingi 127 huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 115, nyongeza ya shilingi 15 kwa bidhaa hizo. Naibu Nais William Ruto ameelezea imani yake kuwa serikali itazingatia kilio cha wananchi.

"Tutaketi chini na bunge ili tuelewane, tuwe na mipango ya kutafuta kodi ya kuendesha maendeleo ya Kenya lakini pia tuhakikishe kuwa Wakenya wengi wanyonge wasifinywe ili tuwe na balance," amesem Naibu Rais William Ruto.

Kenia - Stoffbeutel in Markt (picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim)

Wananchi walalamika kupanda bei za bidhaa

Licha ya bunge kupitisha kodi hiyo ya asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta mwaka 2013, huku utekelezaji wake ukiwa umepangiwa kuanza Septemba 1, 2016 lakini uliahirishwa hadi Agosti 1, na kisha kwa mara nyengine tena bunge likataka uendelee kuahirishwa. 

Wabunge 150 walitarajiwa kukutana kujadili jinsi ya kulegeza mzigo huo kwa mwananchi wa kawaida pamoja na kujadili utendajikazi wa Waziri wa Fedha Henry Rotich, ambaye ameidhinisha utekelezaji wake licha ya bunge kusitisha utekelezaji huo. Hata hivyo mkutano huo haukufanyika, na badala yake Adan Duale, kiongozi wa wengi bungeni amewakosoa vikali wabunge hao.

"Nikiona wabunge wanatoa machozi karibu na raia huo ni unafiki. Mkenya akilia kuwa mafuta yameongezwa hiyo ni haki. Nimeona mwengine ameniandikia barua ati niitishe kikao. Kwa sasa mswada uko na rais. Kwa hivyo wabunge waache unafiki," Adan Duale.

Kodi hiyo ni moja ya njia za kujaza mapengo kwenye bajeti inayopigiwa debe na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF. Kenya inadaiwa shilingi trilioni 5.1, ikimaanisha kuwa kuwa kila Mkenya anadaiwa shilingi laki moja hadi muda huu unavyoendelea.