1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majaji wajiunga na maandamano Sudan

Amina Mjahid
24 Aprili 2019

Kwa mara ya kwanza tangu kufanyika maandamano ya nchi nzima Sudan, majaji nchini humo wamesema wataungana na waandamanaji nje ya makao makuu ya jeshi, kulihamasisha jeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3HM3O
Sudan l nach Putsch l  Proteste gegen Militärrat
Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Taarifa kutoka kwa kundi la majaji inasema majaji hao wanatarajiwa kuanza maandamano yao nje ya makahama ya katiba hadi katika makao makuu ya kijeshi, kuunga mkono mabadiliko yanayotakikana ya kuwa na mahakama zenye uhuru.

Wakati hayo yakiarifiwa viongozi wa maandamano hayo wametishia kuandaa maandamano ya taifa zima iwapo watawala wa kijeshi hawatoridhia matakwa yao ya kurejesha utawala wa kiraia.

Hata hivyo baraza hilo la kijeshi linaloshikilia madaraka  limesema limewaalika viongozi wa maandamano kwa mazungumzo katika ikulu ya rais hii leo jioni. Awali wakati wa mkutano na waandishi habari kiongozi mkuu wa upinzani alisema viongozi wa maandamano wanatarajiwa kukutana ana kwa ana na Mkuu wa Baraza la kijeshi Abdel Fattah al-Burhan.

"Tuko tayari kuzungumza na jenerali Burhan na nadhani masuala yetu yatatatuliwa kupitia majadiliano," alisema kiongozi huyo wa upinzani Omar el-Digeir alipokuwa akizungumza na waandishi habari.

Al sisi na wenzake wataka Jeshi la Sudan kupewa muda zaidi kukabidhi madaraka

Ägypten Kairo - Gipfeltreffen
Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi akiwa na wenzake wa Afrika katika mkutano wa kuujadili mzozo wa SudanPicha: Reuters/The Egyptian Presidency

Jumapili iliyopita viongozi wa maandamano ya kutaka mabadiliko ya kidemokrasia na kisiasa nchini humo walisema wameyaahirisha mazungumzo yao na baraza la kijeshi baada ya kudai kuwa linaendeleza matakwa ya serikali iliyopita iliyoongozwa na rais aliyepinduliwa madarakani mnamo Aprili 11 Omar Hassan al Bashir.

Jeshi lilimuondoa al-Bashir madarakani baada ya miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya utawala wake wa kiimla. Maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakipiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, wakitaka viongozi wapya wa kijeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

Waandamanaji hao wamepata uungwaji mkono kutoka Marekani inayotaka pia jeshi likabidhi mara moja madaraka kwa serikali ya kiraia. Lakini hapo jana viongozi wa kiafrika waliokusanyika nchini Misri katika mkutano ulioitishwa na rais Abdel Fattah al-Sisi, walilisisitiza haja ya Sudan kupewa muda zaidi wa miezi mitatu kwa jeshi hilo kukabidhi madaraka.

Hata hivyo Umoja wa Afrika mnamo Aprili 15 ulitishia kuiondoa sudan katika Umoja huo iwapo itashindwa kukabidhi madaraka hayo ndani ya muda wa siku 15.