Maisha katika kituo cha kuwahudumia wastaafu nchini Ujerumani | Masuala ya Jamii | DW | 29.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Maisha katika kituo cha kuwahudumia wastaafu nchini Ujerumani

Idadi ya watu wanaotumbukia katika hali ya umaskini uzeeni inazidi kuongezeka na wengi kati yao ni wanawake.

Wazee wastaafu wanafanya mazowezi katika kituo cha akuwatunza wazee

Wazee wastaafu wanafanya mazowezi katika kituo cha akuwatunza wazee

Hata Ujerumani umaskini wa uzeeni ni tatizo na ni tatizo linalotishia kuzidi makali miaka inayokuja.Wanawake wanaowalea watoto wao peke yao,watu wanaojituma na ambao mara nyingi wanaranda toka mradi mmoja hadi mwengine,wafanyakazi wa muda mfupi na vibarua,yaani wale watu ambao pato lao halizidi Euro 400,wasomi ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa wakifanya mafunzo kwa mishahara duni-orodha ya watu wanaokabiliwa na hatari ya kuangukia katika hali ya umaskini ni ndefu.Mwaka 2011,asili mia moja nukta tatu ya wastaafu nchini Ujerumani wamekuwa wakiishi kwa ruzuku ya serikali-miaka ijayo idadi yao inasemekana itaongezeka.Serikali kuu ya Ujerumani inajadiliana hivi sasa kuhusu "ruzuku" maalum kuwasaidia watu waliostaafu ambao licha ya kufanya kazi kwa muda wa miaka 40,lakini malipo yaao ya uzeeni hayawatoshi kuweza kuishi ipasavyo.Yeyote yule yule anaeishi kwa Euro takriban 700 anaangaliwa kuwa ni mtu anaekabiliwa na hatari ya kukumbwa na umaskini.

Wastaafu wanaoishi kwa ruzuku ya serikali wanakuwa na Euro 100 tu kama fedha taslimu mfukoni mwao.Kishindo kikubwa zaidi kinakuwa wakati kama huu wa pirika pirika za kabla ya siku kuu ya X-Mass ambapo wakuu wa vituo vya kuwahudumia wazee waliostaafu wanajishughulisha na kupamba vituo hivyo kwa mataa ya rangi rangi na mapambo ya X-Mas na harufu za vitamtam maalum vya X-Mas zikihanikiza ,kuna baadhi ya wazee katika kituo hicho ambao hawamudu kununua zawadi za X- Mas.

"Tatizo linakuwepo kama kuna watoto,wajukuu na wengineo ambapo tunalazimika kusema:la haiwezekani kununua hivi sasa kwasababu kwasasa hakuna kitu."...

Anasema Irina Suchan anaeongoza huduma za jamii katika kituo hicho cha kuwahudumia wazee kilichoko nje kidogo ya mji wa Bonn.Karibu thuluthi moja ya wazee 80 wanaoishi katika kituo hicho wanategemea ruzuku,kuanzia fedha wanazopatiwa walemavu wasioona hadi kufikia msaada wa jamii.Msaada wa jamii ni Euro 100 mzee anazolipwa na ambazo mara nyingi zinamalizika baada ya kununua vidonge vya maumivu kwa mfano Aspirin na kuzungumza kwa simu na mjukuu. Kituo cha huduma za jamii inamaanisha pia mahala ambako wazee wanakwenda kuchukua fomu kwaajili ya kutuma maombi yao wanapohitaji hiki au kile mfano shumizi au koti la baridi.Bibi Suchan anawasaidia kama anavyoweza wazee wanapotaka kujaza fomu hizo.

"Bila ya shaka mara nyingi kunakuwa na mabishano,Kuna wanaohoji :nimefanya kazi muda wote,kwanini hivi sasa niambiwe ,kwanini niachie yote haya.Rahisi zaidi ni pale maombi hayo yanapohusika na fedha za kulipia makaazi na kuwatunza.Kwasababu maombi kama hayo husikika vyengine kuliko ningesema kwa mfano tunabidi sasa tujaze fomu ya kuomba msaada wa jamii.Kwasababu fomu kama hiyo ni ya aina yake hasa kwa wale ambao haraka wanapandisha mori."

Altersheim für Demenzkranke Hogewey, Niederlande

Bibi mtumzima anakwenda kununua vitu

Viongozi wa kituo hicho tu ndio wanaojua nani kati ya wazee anapokea msaada wa jamii.Kuna wakfu moja iliyojitolea kuwalipia gharama za simu pamoja na zile zinazotokana na mipango ya kuwateembeza wazee.Irina Suchan aliwauliza kisiri siri watatu kati ya wazee wanaoishi katika kituo hicho kama watakubali kuhojiwa na DW-wote watatu wamekataa.Wanaona haya,anasema mtaalam huyo wa masuala ya jamii.Na wana wasi wasi pia wengine wasije wakajua kwamba wao ni maskini.

Ndani kuna kitanda na chuka za rangi ya urujuani ,viti viwili na mito yenye rangi za kupendeza zinazooana na shuka na ukutani zimetundikwa picha ya watu wanaotabasamu .

"Bibi huyu amehamia mwaka huu .Hiki ni kisa cha kawaida.Daima alikuwa akifanyakazi katika hospitali ya mumewe..Waliishi muda mrefu Damascus,wamerejea kuja kuishi Ujerumani katika miaka ya 70 na wote wawili,si mume wala si mke,hakuna aliyelipa katika bima ya uzeeni."

Barazani Irina Suchan ametonyesha bibi mmoja ambae nguo alizovaa pia zina rangui ya urujuani.Anamnong'onea mwenzake.Wanawake ndio wanaoathirika zaidi na hali ya umaskini wa uzeeni."Kuna wengi miongoni mwa hirimu hii waliokubali kurejeshewa fedha walizochangia katika bima ya uzeeni waalipokuwa wanafunga ndowa-ilikuwa katika miaka ya 50 na 60.Ili kuweza kugharimia harusi mwanamke ndie aliyekuwa akirejeshewa pesa kutoka fuko la uzeeni."

Anne Hoffman und ihre Großmutter

Bibi mtumzima anatembelewa na jamaa yake

Ingawa wanawake wengi wanaendelea kufanya kazi,hata hivyo bado wanakabailiwa na kitisho cha kumaliziokia katika hali ya umaskini,anasema Sabine Graf-naibu kiongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi vya Ujerumani katika jimbo la North Rhine Westfalia:

"Sehemu kubwa ya wanaokumbwa na hatari ni wanawake-mishahara yao ni haba,kwa hivyo wanachangia kidogo pia katika bima ya uzeeni.Mpaka sasa bado mshahara anaopokea mwanamme unapindukia asili mia 20 ya mshahara wa mwanamke .Kwa hivyo mchango haba katika fuko la bima ya uzeeni ndipo chanzo cha na malipo haba ya uzeeni.Kwa hivyo wao ndio wanaokabiliwa na hatari ya kuangukia katika hali ya umaskini."

Lakini hata watu wanaojituma wenyewe,wanaoranda randa toka mradi mmoja hadi mwengine,watu wanaofanya kazi za muda mfupi na vibarua wanakabiliwa na hatari ya kuanagukia katika hali ya umaskini,sawa na watu wenye familia kubwa au wale wanaowalea watoto wao peke yao.Sabine Graf anasema wanakadiria thuluthi moja ya wastaafu,wake kwa waume watajikuta wakiishi katika hali ya umaskini siku za mbele-Hicho ni kishindo kwa nchi kama hii ya Ujerumani na balaa kubwa kwa wahusika."

Irina Suchai anaamini atakapokuwa mzee hatoweza kumudu kujilipia gharama za kuhudumiwa katika kituo kama hiki.Hadi atakapostaafu,anaamini Ujerumani haitakuwa tena pengine na uwezo wa kugharimia vituo vya kuwatunza wazee.Anasaema katika vituo kama hivi katika mkoa wa Ruhr marafiki zake wanakofanya kazi,asili mia 60 mpaka 70 ya wazee wastaafu wanaishi kwa kutegemea msaada wa jamii.

Mwandishi:Conrad,Naomi/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com