1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Misri yaifuta kamati ya katiba

10 Aprili 2012

Mahakama nchini Misri imelifuta jopo la wajumbe 100 lililoteuliwa na bunge kuandika katiba mpya ya nchi hiyo, kufuatia ombi la wanasheria waliodai kuwa uamuzi wa bunge kuteua wajumbe wake haukuwa jambo sahihi.

https://p.dw.com/p/14aMS
Bunge la Misri
Bunge la MisriPicha: dapd

Uamuzi wa Jaji Ali Fekri umepinga hoja ya serikali na bunge kwamba mahakama yake haina uwezo wa kushughulikia masuala ya kikatiba, na badala yake umesema wazi kwamba "kamati ya katiba iliyoteuliwa na bunge haina uhalali."

Kesi hii ni moja kati ya malalamiko mengi yaliyoko mahakamani yanayotaka kuvunjwa kabisa kwa bunge kwa sababu haliwakilishi watu wa Misri. Mwanasheria Khaled Abu Bakr, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, uamuzi wa leo wa mahakama "unasitisha pia shughuli za bunge hadi hapo litakapotolewa tangazo jengine baada ya jopo la majaji kukutana".

Naye Essam Sultan, mmoja wa wanasheria walioishitaki kamisheni ya katiba mahakamani, ameliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kuwa hivi punde uamuzi huo wa mahakama utakuwa umeshawasilishwa bungeni, lakini cha msingi ni kwamba kuanzia sasa kamati hiyo haina tena uhalali wa kisheria.

Pigo kwa Udugu wa Kiislamu

Hukumu hii ni pigo kubwa kwa vyama vya kisiasa vinavyofuata misingi ya dini ya Kiislamu nchini humo, ambavyo vinaonekana kudhibiti siasa za nchi hiyo tangu kuondolewa madarakani kwa Hosni Mubarak miezi 14 iliyopita.

Mbunge wa chama cha Haki na Uhuru cha Misri bungeni.
Mbunge wa chama cha Haki na Uhuru cha Misri bungeni.Picha: picture-alliance/dpa

Hoja kubwa iliyowasilishwa na upande wa walalamikaji, ni kwamba uchaguwaji wa wajumbe wa kamati hiyo ulivunja tamko la katiba iliyopita kwenye kura ya maoni ya mwaka jana.

Kwa mujibu wa katiba ya muda ya Misri, bunge ndilo lenye haki ya kuteua kamati ya katiba, lakini haisemi wazi ikiwa wabunge wanaweza kuwa wajumbe wa kamisheni hiyo ama la.

Katika kile kinachoonekana ni kutokana na tafauti za kiitikadi, wajumbe vyama vya kiliberali na taasisi rasmi za Kiislamu na Kikristo, ambao walishiriki kuuondoa utawala wa Mubarak, wamejiondoa kwenye kamati hiyo, wakilalamikia kwamba inatawaliwa na watu wenye misimamo mikali ya Kiislamu. Asilimia 60 ya wajumbe wa kamati hiyo wanatoka kwenye vyama vyenye kufungamana na dini ya Kiislamu.

"Kamati ni sauti wa Wamisri wote"

Hata hivyo, Chama cha Uhuru na Haki, ambalo ni tawi la kisiasa la kundi la Udugu wa Kiislamu, kimesema kwamba kamati hiyo iliyoteuliwa na bunge inawakilisha jamii nzima ya Misri. Chama hicho ndicho chenye wingi wa viti bungeni.

Mbunge wa chama cha Salafi cha Misri bungeni.
Mbunge wa chama cha Salafi cha Misri bungeni.Picha: dapd

Dhana kwamba kundi la Udugu wa Kiislamu lina nia ya kuchukuwa madaraka na kuzitawala siasa za Misri ndizo zinazooneakana kuwa sababu kubwa ya vyama vya kiliberali na wafuasi wao kuchukuwa kila hatua kuzuia hilo lisitokee.

Wiki iliyopita Udugu wa Kiislamu ulitangaza rasmi kumsimamisha mgombea wao kwenye uchaguzi ujao wa rais, ikiwa ni kinyume na ahadi ya kutoweka mgombea lililoweka hapo mwanzoni.

Katiba mpya ya Misri ndiyo ambayo ilitarajiwa iamue nguvu za rais na pia hatima ya jeshi nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman