1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAsia

Mahakama India yaondoa mfumo usio wazi wa ufadhili kisiasa

Bruce Amani
15 Februari 2024

Mahakama ya juu ya India imeufutilia mbali mfumo wa kufadhili uchaguzi uliodumu kwa miaka saba ambao uliwaruhusu watu na makampuni kutoa michango isiyo na kikomo na isiyojulikana inakotoka, kwa vyama vya kisiasa.

https://p.dw.com/p/4cRvj
India, Neu Delhi | Kiongozi wa upinzani India  Rahul Gandhi
Kiongozi wa upinzani India Rahul GandhiPicha: Altaf Qadri/AP/picture alliance

Mahakama imesema mfumo huo unakwenda kinyume cha sheria. Uamuzi huo umeonekana kama pigo kwa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi cha Bharatiya Janata, ambacho kimekuwa mnufaika mkubwa zaidi wa mfumo huo ulioanzishwa mwaka wa 2017.

Mfumo huo unaoitwa Dhamana za Uchaguzi, ulipingwa na wanachama wa upinzani na asasi za kiraia kwa madai kuwa unazuia haki ya umma kujua nani ametoa fedha kwa vyama vya siasa.

Chini ya mfumo huo, mtu au kampuni ingeweza kununua hati za dhamana kutoka Benki ya Taifa ya India na kutoa kama mchango kwa chama cha kisiasa.

Soma pia:Polisi wamwagwa India kuwakabili wakulima wasiandamane

Mahakama hiyo yenye majaji watano ikiongozwa na Jaji Mkuu D. Y. Chandrachud imesema michango ya kisiasa inampa mchangiaji nafasi ya ushawishi katika masuala ya kutunga sera.