1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wakimbizi wa Tigray wakimbilia Sudan

Grace Kabogo
11 Novemba 2020

Mzozo uliosababisha mauaji kwenye jimbo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia umesambaa hadi kwenye eneo la mpakani, huku maelfu ya watu wakikimbilia Sudan, wakiwemo wanajeshi wanaotafuta ulinzi.

https://p.dw.com/p/3l8bx
77 Percent Äthiopien Vertreibung Flüchtlingslager in Dilla
Wakimbizi katika kambi ya Dilla Ethiopia, familia 200 wanaishi katika jengo mojaPicha: DW/M. Gerth-Niculescu

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ameikataa miito ya kimataifa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa jimbo la Tigray, akisema kuwa hatofanya mazungumzo hadi  ''operesheni za utekelezaji wa sheria '' zitakapomalizika. Anataka kuwakamata viongozi wa serikali ya jimbo la Tigray, ambao anawaona sio halali, huku akiliharibu ghala lao lililojazwa silaha za kivita.

Ingawa Uingereza na Umoja wa Afrika umemtaka mara moja asitishe mashambulizi, Abiy ameapa kuwa jeshi litafanikiwa kuumaliza mara moja mzozo wa Tigray. Lakini wataalamu wanaonya kuwa mzozo huo unaweza kusabaisha kukosekana utulivu na kulidhoofisha taifa hilo la Afrika. Soma Zaidi Umoja wa Afrika wataka mapigano yasitishwe Tigray, Ethiopia

Kumiminika mwa wakimbizi ni ishara ya kwanza inayoonyesha kuongezeka kwa mzozo wa kibinaadamu unaowaathiri mamilioni ya watu katika Pembe ya Afrika. Tigray inabakia bila ya kuwa na mawasiliano na ulimwengu kwa takriban wiki nzima sasa, baada ya mawasiliano kukatwa na Abiy kutangaza kuwa jeshi linaendesha operesheni kujibu mashambulizi dhidi ya kambi ya jeshi.

Umoja wa Mataifa na washirika wa Sudan wanajiandaa kuwapokea wakimbizi 20,000. Mmoja wa wanadiplomasia kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, amesema kuwa hadi sasa mamia ya watu wameripotiwa kuuawa katika pande zote mbili zinazohasimiana. Bado sio rahisi kuthibitisha madai ya kutoka upande wowote.

Uingereza yaongeza shinikizo 

Äthiopien Militärparade in Tigray
Vikosi maalum vya Tigray vikionekana katika mitaa ya mji mkuu wa mkoa huo, MekelePicha: DW/M. Hailesilassie

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab ameongeza shinikizo kwa Abiy, akisema kuwa amezungumza na waziri mkuu na kumsihi wajizuie na mashambulizi zaidi. Raab amesema raia wanapaswa kulindwa na msaada wa kibinaadamu unatakiwa uruhusiwe kuwafikia wananchi.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya amani pamoja na mapigano kusitishwa mara moja Tigray. Moussa amesema umoja huo uko tayari kuunga mkono juhudi za Waethiopia katika kutafuta amani. Soma zaidi Mvutano wa nchini Ethiopia

Mkuu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi nchini Sudan, Alsir Khaled amesema takriban wakimbizi 3,500, wakiwemo wanawake na watoto wamewasili kwenye jimbo la Kassala nchini Sudan. Shirika la habari la Sudan, SUNA limeripoti kuwa wanajeshi wapatao 30 wa Ethiopia waliungana na wakimbizi kukimbilia Sudan.

Wakati huo huo, mlipuko mkubwa chini ya daraja kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa umemjeruhi mtu mmoja na kusababisha apoteze mguu wake mmoja. Msemaji wa polisi wa Ethiopia amesema leo kuwa hakuna ishara yoyote kwamba mlipuko huo unahusika na mzozo unaoendelea Tigray ambako majeshi ya serikali ya shirikisho yanapambana na majeshi ya jimbo hilo la kaskazini.

 

(AP, AFP, Reuters)