1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Macron asema IS imehusika katika shambulizi la Moscow

Tatu Karema
25 Machi 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema dalili zote zinaashiria kuwa kundi linalojiita dola la kiislamu IS limehusika na shambulizi kwenye ukumbi wa tamasha mjini Moscow ambapo watu 137 waliuawa

https://p.dw.com/p/4e6QX
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akitoa hotuba mjini Sainte-Savine-Le-Lac, Kusini Mashariki mwa Ufaransa mnamo Machi 30,2023
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Sebastien Nogier/AP/picture alliance

Rais Macron amesema IS imedai kuhusika na shambulizi hilo la Moscow na habari walizo nazo, pamoja na taasisi za kijasusi na washirika wao,  zinaashiria kuwa shambulizi hilo limefanywa na kundi hilo.

Macron pia amesisitiza uungaji mkono na mshikamano na watu waUrusi na pia kuwapa pole waathiriwa wote na familia zao pamoja na wale waliojeruhiwa.

ISIS-K ilijaribu kufanya mashambulizi nchini Ufaransa

Macron amesema kwamba tawi la IS nchini Afghanistan linalojulikana kama ISIS-K, lililodai kuhusika katika shambulizi hilo la Moscow, pia lilijaribu kufanya mashambulizi nchini Ufaransa.

Rais huyo ameongeza kuwa hali hii inaeleza sababu ya Ufaransa siku ya Jumapili, kutoa tahadhari ya juu ya ugaidi kufuatia shambulizi la Moscow. Macron alikuwa akizungumza wakati wa ziara katika eneo la Guiana nchini Ufaransa.

Soma pia:Watu 4 washitakiwa kwa kuhusika na shambulio la Moscow

Katika tamko lake kuhusu shambulizi hilo, Rais wa Urusi Vladimir Putin hakuzungumzia hadharani kuhusika kwa kundi hilo la IS na washambuliaji ambao amesema walikuwa wanajaribu kutorokea Ukraine.

Putin amesema kuwa baadhi ya watu kutoka upande wa Ukraine walikuwa wametayarishwa kuwasaidia washambuliaji hao baada ya kuvuka mpaka .

Rais wa Urusi Vladimir Putin akilihutubia taifa mnamo Machi 23,2024 kufuatia shambulizi kwenye ukumbi wa tamasha wa Crocus mjini Moscow
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Kremlin.ru/REUTERS

Ukraine imekanusha kuhusika katika shambulizi hilo huku Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskiy akimshtumu Putin kwa kujaribu kubadili mwelekeo wa shtuma zinazotokana na shambulizi hilo kwa kuitaja Ukraine.

Urusi imepinga madai ya Marekani na mataifa mengine kwamba wanamgambo wa IS walipanga mashambulizi hayo ya Ijumaa na kuishtumu nchi hiyo kwa kuegemea upande wa Ukraine.

Ukraine yasema uharibifu uliosababishwa na Urusi wafikia mabilioni ya pesa

Waziri wa nishati wa Ukraine  German Gerashchenko, amesema leo kuwa uharibifu uliosababishwa na shambulizi kubwa la Urusi dhidi ya viwanda vyake vya nishati huenda ukafikia mabilioni ya pesa. Hata hivyo waziri huyo hakutaja sarafu ya kiwango hicho.

Gerashchenko amewaambia wanahabari kwamba wanahitaji muda zaidi kukadiria uharibifu huo kwasababu kuna kiwango kikubwa cha taka.

Soma pia:Kremlin kwa mara ya kwanza yaitaja operesheni ya Ukraine kuwa vita

Ukraine inasema wiki iliyopita, Urusi ilifanya shambulizi kubwa la anga kwa kufyetua makombora 90 na droni 60 dhidi ya viwanda vya nishati kote nchini humo na kusababisha vifo vya takriban watu watano.

Gerashchenko ameyatajamashambulizi hayo kuwa makubwa zaidi tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini humo mnamo Februari mwaka 2022.

Benki ya dunia imekadiria gharama ya ujenzi mpya unaoikabili Ukraine, zaidi ya miaka miwili baada ya vita kuanza nchini humo, kuwa takriban dola bilioni 486.