1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yawaweka kizuizini washukiwa wa ugaidi

Tatu Karema
25 Machi 2024

Urusi imeamuru wanaume wanne wanaoshutumiwa kuuwa watu wasiopungua 137 kwenye tamasha mjini Moscow wawekwe kizuwizini kwa mashtaka ya ugaidi wakati watu zaidi ya 100 wakiwa wamelazwa hospitalini

https://p.dw.com/p/4e5W1
Mshukiwa mmoja wa shambulizi mjini Moscow afikishwa katika mahakama ya Basmanny mjini Moscow mnamo Machi 24,2024
Mshukiwa mmoja wa shambulizi mjini Moscow afikishwa mahakamaniPicha: Shamil Zhumatov/REUTERS

Katika mfululizo wa vikao vya mahakama vilivyofanyika usiku kucha mjini Moscow na vilivyoendelea hadi alfajiri ya leo, wanaume hao waliokuwa na majeraha ya uso, walifikishwa katika mahakama ya Basmanny iliyokuwa imejaa waandishi wa habari.

Maafisa wa idara ya usalama ya Urusi, FSB walimsukuma mmoja wa wanaume hao kwa kutumia kiti cha magurumu kufuatia ripoti na video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya Urusi za kufanyika kwa mahojiano yalioghubikwa na mateso baada ya watu hao kukamatwa siku ya Jumamosi.

Soma pia:Watu 60 wauawa kufuatia shambulizi kwenye tamasha la muziki

Wanaume hao wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela ijapokuwa maafisa wa Urusi wamelalamika kuhusu kuondolewa kwa muda kwa adhabu ya kifo ili kutoa hukumu kali zaidi.

Putin aashiria Ukraine imehusika katika shambulizi la Moscow

Katika matamshi pekee kwa umma tangu kutokea kwa shambulizi hilo, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitaja kuhusika kwa Ukraine, akisema kuwa washambuliaji hao wanne walikamatwa walipokuwa wakijaribu kutoroka.

Kundi linalojiita dola la kiislamu IS limedai kuhusika katika shambulizi hilo la Ijumaa jioni ijapokuwa maafisa wa Urusi hawajatoa tamko kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa kundi hilo.

Ukraine yasema Urusi imeshambulia maeneo yake ya Kusini

Ukraine imesema Urusi imeshambulia maeneo ya Kusini ya Mykolaiv na Odesa kwa droni  huku nchi hizo mbili zikielendeleza mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya usiku kucha dhidi ya viwanda vya nishati .

Maafisa wa uokoaji katika eneo la shambulizi la Urusi mjini Kyiv nchini Ukraine mnamo Machi 25,2024
Maafisa wa uokoaji katika eneo la shambulizi la Urusi mjini Kyiv, UkrainePicha: Gleb Garanich/REUTERS

Katika taarifa aliyochapisha mapema leo katika mtandao wa kijamii wa Telegram, gavana wa Odesa Oleg Kiper, amesema kwa mara nyingine tena, Urusi imeshambulia eneo hilo la Odesa kwa droni .

Kiper ameongeza kuwa miundo mbinu ya nishati imeharibiwa na umeme kukatika katika baadhi ya maeneo ya mji huo.

Wakati wa mahojiano kwenye televisheni ya kitaifa, msemaji wa jeshi la Ukraine Nataliya Gumenyuk, amesema watu 11 walijeruhiwa katika mji wa Kusini wa Mykolaiv .

Soma pia: Urusi yafanya mashambulio ya Droni katika mji Odessa

Nchini Urusi, moto ulizuka katika kiwanda kimoja cha umeme katika eneo la Kusini la Rostov baada ya mfululizo wa mashambulizi ya droni za Ukraine katika eneo hilo. Haya ni kulingana na gavana wa eneo hilo Vasily Golubev.

Soma pia:Urusi yaangusha makombora yaliyorushwa kwenye mikoa yake

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, Golubev amesema umeme ulikatika katika vituo viwili vya umeme kwenye kiwanda cha umeme cha Novocherkassk, moja ya viwanda vikubwa Kusini Magharibi mwa Urusi.

Hata hivyo Golubev ameongeza kuwa hakukuwa na majeruhi.

Urusi imeripoti kudungua droni 11 za Ukraine katika eneo hilo la Rostov.