1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron akosolewa kwa sheria ya kuwasaidia watu kufa

Bruce Amani
11 Machi 2024

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anakabiliwa na ukosoaji kutoka kwa wahudumu wa matibabu, wapinzani wa kisiasa na Kanisa Katoliki kuhusiana na rasimu ya muswada wa sheria inayoruhusu kuwasaidia watu kufa.

https://p.dw.com/p/4dOjb
Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Gonzalo Fuentes/AFP/Getty Images

Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa bungeni mwezi Mei na kama utapitishwa, utaruhusu kusaidiwa kufa kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hali mahututi.

Macron ameyaambia magazeti kuwa mswada huo utajumuisha "masharti makali" kuhusu kuwaruhusu watu kujichoma wenyewe sumu au kumuomba mwanafamilia au mhudumu wa matibabu kama hawawezi kujifanyia hivyo.

Hatua hiyo inajiri baada ya bunge la Ufaransa wiki iliyopita kuweka katika katiba ya nchi haki ya kutoa mimba na kuwa ya kwanza ulimwenguni kufanya hivyo.

Macron alikuwa mpiganiaji mkubwa wa "haki" hiyo.

Lakini katika taarifa ya pamoja waliyoitowa siku ya Jumatatu (Machi 11), mashirika ya wauguzi na watoa huduma kwa wagonjwa wa saratani wamesema wamefadhaishwa, kukasirishwa na kuhuzunishwa na mpango huo.